Na mwandishi wetu
Kocha wa Geita Gold, Fred Felix Minziro amejinasibu kutojali kuwa ugenini keshokutwa dhidi ya Coastal Union na badala yake ametamba kuwa atatafuta matokeo ya ushindi mbele yao.
Geita itakuwa ugenini Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ikipambana kutafuta matokeo ya ushindi kwa mechi ya pili mfululizo msimu huu baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Polisi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Minziro amefunguka kwamba kikubwa wanachohitaji wao ni ushindi tu sasa hakuna kingine hivyo watakwenda kupambana bila ya kujali kama wapo ugenini au la.
“Kikubwa ni kutafuta matokeo bila kujali kama kocha ni nani au tunacheza na timu gani au kama tupo ugenini, sisi tumejipanga kwa mapambano, tunahitaji matokeo ndiyo kitu muhimu kwetu kwa sasa kuliko kuangalia tunacheza wapi,” alisema Minziro.
Geita ambayo msimu uliopita ilimaliza kwenye nafasi ya nne, mpaka sasa ipo nafasi ya 12 ikiwa na pointi sita baada ya mechi sita. Geita imeshinda mechi moja, imefungwa mara mbili na kupata sare tatu.
Naye Ofisa Habari wa Coastal Union, Jonathan Tito alibainisha kuwa kikosi hicho kilicho chini ya kocha Mkenya, Yusuf Chipo kipo tayari kwa mchezo huo baada ya kwenda nje ya mkoa wa Tanga kwa siku nane kujiweka madhubuti.
“Tulikuwa nje ya mkoa kwa siku nane na kocha ameridhika kwa kile kilichofanyika huko, tumejipanga kwa ajili ya mechi hiyo na mechi zote za ligi kwa maana kocha amekuja katikati na alitaka apate muda angalau kidogo akisuke sawasawa kabla ya mechi ya Geita, tupo tayari,” alisema Tito.
Msimu uliopita ambao ulikuwa wa kwanza kwa Geita kushiriki Ligi Kuu Bara, iliifunga Coastal mabao 2-0 kabla ya kutoa sare ya 1-1 kwenye mechi ya pili iliyopigwa Mkwakwani, Tanga, ingawa Tito amesisitiza hayo hayatajirudia tena msimu huu.
Soka Minziro apiga hesabu za ushindi kwa Coastal
Minziro apiga hesabu za ushindi kwa Coastal
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
