London, England
Klabu ya Manchester City inahaha kuhakikisha beki wake, John Stones anakuwa fiti kabla ya Manchester Derby itakayopigwa Jumapili kwenye dimba la Etihad.
Stones, 28, alipatwa na matatizo ya misuli na kulazimika kutoka nje kipindi cha kwanza wakati wa mechi ya England na Ujerumani ya Uefa Nations Ligi iliyochezwa Jumatatu kwenye Uwanja wa Wembley na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Baada ya Stones kuumia mabosi Man City tayari wameandaa utaratibu ili Jumatano mchezaji huyo awe Manchester kwenye makao makuu ya klabu hiyo ili kufanyiwa uchunguzi wa kina na timu ya madaktari wa klabu kabla ya kujua kama ataiwakilisha timu hiyo katika mechi hiyo ya Jumapili dhidi Man United.
Stones alicheza mechi mbili za Man City zilizopita katika nafasi ya beki wa kulia baada ya Kyle Walker kuumia. Mara ya mwisho Walker aliiwakilisha City Septemba 3 katika mechi dhidi ya Aston Villa lakini aliiwakilisha England Jumatatu katika mechi dhidi ya Ujerumani na bila shaka Jumapili atakuwa fiti kuivaa Man United.
Man City pia ina uhakika matibabu ya Kalvin Phillips yanakwenda vizuri baada ya mchezaji huyo kufanyiwa operesheni mapema wiki hii baada ya kuumia akiwa kwenye mazoezi kabla ya mechi yao dhidi ya Wolves.
Phillips alijitoa katika mechi za England za Uefa Nations Ligi dhidi ya Ujerumani na Italia na uwezekano wa kuwamo katika kikosi cha England kitakachoshiriki fainali za Kombe la Dunia ni mdogo.
Kocha wa England, Gareth Southgate, Oktoba 20 anatarajia kutaja kikosi chake kitakachokwenda Qatar kwenye fainali za Kombe la Dunia ambapo timu hiyo itatupa kete yake ya kwanza Novemba 12 dhidi ya Iran.
Kimataifa Stones aipasua kichwa Man City
Stones aipasua kichwa Man City
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
