Na Jonathan Haule
Kuachwa kupo na kunaumiza, je ni ipi njia sahihi ya kuachana baada ya mapenzi kuwa moto moto? Ni sahihi kumtamkia mpenzi wako bila kupepesa kwamba humtaki? Je ni sahihi kumkwepa na kumhadaa mpenzi wako hadi mwenyewe ajue kwamba amechokwa?
Mapenzi yanapokuwa moto moto ni vigumu kuamini kwamba wanaopendana wanaweza kuchokana na kuamua kuachana iwe ni kwa mmoja kumkosea mwenzake au kwa sababu yoyote ile lakini kuachana kupo na wapenzi wengi hupata tabu pale inapofikia hatua ya mtu mmoja kumchoka mwenzake.
Kuna baadhi ya watu hasa wa tamaduni za kimagharibi, suala la kuachana kwao ni jambo dogo tu, mtu haoni tabu kumwambia mpenzi wake amemchoka na anataka waachane, kazi ipo kwa mila zetu, kuachana kunaandamana na unafiki, unajifanya unampenda lakini huonyeshi mapenzi, badala yake unamfanyia hadaaa na kumuonyesha dalili zote za kumchoka.
Ulikuwa unampigia simu kila siku lakini taratibu simu zinaanza kupungua, badala ya kila siku inakuwa kila baada ya siku mbili au tatu, ukilalamika unapigiwa simu siku mbili mfululizo halafu baada ya hapo kupigiwa simu ni kwa wiki mara moja.
Mtu wa aina hii ni kwamba amekuchoka lakini anapata tabu kukwambia kwamba amekuchoka badala yake anaamua kuwa mnafiki, anajifanya anakupenda kumbe hakupendi lakini hana ujasiri wa kukutamkia kwamba hakupendi, anatafuta sababu ya kukukasirisha ili muachane.
Katika matukio ya aina hii neno niko ‘busy’ ndio silaha kuu ya kumkwepa mpenzi, “Mbona nimekupigia simu hupokei?” “Niko busy, mambo mengi.” Chenga za aina hii tunapigana sana pale tunapochokana.
Mlikuwa na utaratibu wa kutoka ‘out’ kwa wiki japo mara moja, hali hiyo inapotea ghafla na unapouliza kulikoni, jibu ni rahisi tu, ”niko busy”. Kuwa busy huku kunakokuja ghafla ni unafiki fulani unaotokana na kushindwa kumwambia mpenzi wako kwamba umemchoka au humtaki na ni bora muachane.
Hata hivyo si wote ambao wanashindwa kuwatamkia wapenzi wao kwamba wamewachoka au wanataka waachane ni wanafiki, wakati mwingine ni kukosa ujasiri wa kutamka neno la kuachana kwa sababu mbalimbali, moja ni kumfikiria yule unayemwambia ataichukuliaje hali hiyo.
Na hapa kinachotusumbua ni mazingira ya mapenzi yanapokuwa moto, hasa unapokumbuka kwamba uliwahi kumwambia yeye ndio kila kitu, bila ya yeye maisha hayaendi, huoni husikii kwake, unapokumbuka matukio ya aina hii nafsi inakusuta na kuamua kumpiga chenga ili tu muachane au unamtengenezea matukio ili akikosea akanasa kwenye matukio yako hiyo inakuwa sababu ya kuachana.
Kingine ambacho kinatutesa na kuona tabu kumtamkia mtu kwamba umemchoka na unataka muachane ni fadhila, kwa kiasi kikubwa wanaoumizwa na fadhila hizi ni wanawake, kutokana na mambo mengi wanayofanyiwa wakati mapenzi yakiwa moto hata wanapomchoka mwanaume na kutaka waachane kinachofanyika ni kutengeneza tukio au kukasirika kwa sababu ambayo haina mbele wala nyuma.
Katika mazingira haya mwanaume akikosea akawa mkali na kutoa maneno ya kumkaripia, hapo mwanamke anakuwa amepata sababu tosha ya kujiweka kando na mwanaume, anakuwa ameepukana na ugumu wa kumtamkia mwanaume kwamba hamtaki, badala yake anapata sababu nyingine kabisa ya kuachana na wewe.
Kwa wenzetu wa utamaduni wa Kimagharibi suala la kuachana ni jambo dogo tu, iliwahi kuelezwa kwamba Kanye West alipomchoka mrembo Amber Rose alimwambia moja kwa moja na hatimaye wakaachana, kila mmoja akashika lake.
Kwa upande mwingine wenzetu hawa hawana muda wa kupoteza, akimchoka mtu hahitaji kumpiga chenga, kumtengenezea tukio au unafiki wa aina yoyote, atakachofanya ni kumwambia kila anachoona sahihi bila kujali maumivu atakayomuachia mwenzake.
Ni kawaida kwa wenzetu hawa kumsikia mwanaume akimwambia mwanamke, ‘Do you know that you and me is over’ (Je unajua kwamba mimi na wewe tumefika mwisho) au anaweza akamwambia, I think we have been together for so long, and I feel I am tired, ” (Nafikiri tumekuwa pamoja muda mrefu sasa, na najiona nimechoka.” Kauli hizo na zinazofanana na hizo ndizo za wenzetu wa Kimagharibi.
Jamaa hawa hawana muda wa kudanganyana baada ya kuchokana, mwanamke pia anaweza kuamua tu kumwambia mwanaume kwamba tayari ana mpenzi mwingine na mwanaume akaipokea hali hiyo na kuamua kuangalia mbele.
Kama nilivyosema hapo juu kwamba kuachwa kupo na kunaumiza lakini je ni kuachwa kupi kubaya na kunaumiza zaidi, kuuachwa Kimagharibi kwa kuambiwa bila kupepesa kwamba umechokwa, au kuachwa kwa staili yetu ya kumfanyia mtu hadaa hadi mwenyewe anajigundua kwamba hatakiwi?
Kuna wanaoamini kwamba kuachwa Kimagharibi kunaumiza lakini ni afadhali kwani baada ya muda unapona majeraha ya kuachwa na kusahau kila kitu, lakini kuna wanaoamini kwamba kuachwa kwa staili yetu hii ni afadhali kwa sababu unajipa matumaini, taratibu kadri siku zinavyokwenda matumaini yanafifia siku hadi siku na mwishowe unakubali hali halisi kwamba mwenzako hakutaki, unaamua kuangalia mambo yako.
Tukutane juma lijalo
green.sports82@gmail.com
Mahusiano Kuachwa kwa aina gani kunaumiza zaidi?
Kuachwa kwa aina gani kunaumiza zaidi?
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
