Switzerland
Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) limethibitisha rasmi Jumanne hii uamuzi wa kuifungia Urusi katika kushiriki fainali za Ulaya za 2024 au Euro 2024.
Februari mwaka huu, timu za soka za Urusi zilifungiwa kushiriki mashindano ya soka ya kimataifa na Uefa pamoja na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) baada ya nchi hiyo kuivamia Ukraine kijeshi, uamuzi ambao hata hivyo Urusi iliukatia rufaa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS).
Katika uamuzi mwingine, Uefa iliamua kuiruhusu nchi ya Belarus kuwamo kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kufuzu Euro 2024 na hivyo jina la nchi hiyo kuwamo katika makundi yatakayopangwa na kutangazwa mwezi ujao baada ya Ujerumani kutaka nchi hiyo itolewe kwa kuwa ni mshirika wa kijeshi wa Urusi.
Kwa hiyo Belarus itakuwamo katika nchi zitakazopangiwa makundi ingawa kwa sababu za kiusalama, timu ya Belarus haitopangwa kundi moja na majirani zao wa Ukraine.
Makundi ya nchi shiriki yatakayowania kufusu Euro 2024 yatapangwa na kutangazwa Oktoba 9 mjini Frankfurt, Ujerumani na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Nancy Faeser wiki iliyopita alitoa tamko la kuitaka Uefa kutoiruhusu Belarus kushiriki katika michuano hiyo na tayari Uefa imeshamjibu waziri huyo kwa barua ikimuelezea uamuzi wake wa kuiruhusu nchi hiyo kushiriki Euro 2024.
Uamuzi ambao umechukuliwa na Uefa dhidi ya Belarus ni ule wa kutoruhusu nchi hiyo kuwa mwenyeji wa mechi za soka na kuhakikisha mechi zao za ugenini hata pale wanapokuwa ‘wenyeji’ zichezwe bila ya mashabiki uwanjani.
Uamuzi mwingine wa Uefa ambao unaendelea ni ule wa kuzuia mechi kati ya timu za Azerbaijan na Armenia au Hispania na Gibraltar pamoja na ule unaozizuia timu za Serbia na Bosnia-Herzegovina kucheza dhidi ya timu ya Kosovo.
Kimataifa Uefa yaifuta rasmi Urusi Euro 2024
Uefa yaifuta rasmi Urusi Euro 2024
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
