Na mwandishi wetu
Kocha wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Honour Janza ameita kikosi cha wachezaji 23 huku akimrejesha beki Abdi Banda kwa maandalizi ya michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Libya itakayochezwa nchini Libya wiki ijayo.
katika kikosi hicho ambacho kimejaa sura mpya kimewakosa baadhi ya mastaa waliozoeleka kuitwa mara kwa mara kama Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’, Farid Mussa, Bakari Mwamnyeto, Jonas Mkude, Reliants Lusajo, George Mpole, Kibu Denis na wengine.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, Janza alisema kikosi kilichoitwa kitaingia kambini mwishoni mwa wiki hii na kujifua siku ya Jumatatu kisha Jumanne kitaelekea Libya kwa ajili ya michezo hiyo.
Pia ameeleza michezo hiyo itatumika kwa ajili ya kujiweka imara kabla ya baadaye kuendelea na maandalizi ya mechi za kufuzu fainali za mataifa ya Afrika, Afcon.
Alisema kikosi kilichoitwa kikiwa na baadhi ya sura mpya ni kutaka kuona uwezo na kiwango cha kila mmoja na kwamba bado milango iko wazi kwa wachezaji wengine walioko Ulaya na hapa nchini, wataendelea kuwafuatilia lengo ni kuona wote namna wanavyolipigania taifa.
“Tutaendelea kuwatambua wachezaji wengine, kama nilivyosema kuna wachezaji wako Ulaya na hatuwajui tuleteeni tutawafuatilia, kuna wengine pia wako timu za vijana na wengine hatujawaita nafasi bado ipo,” alisema kocha huyo aliyechukua mikoba ya Kim Paulsen hivi karibuni.
Alisema baadhi ya wachezaji aliowaita na wengine kuwarejesha aliwahi kuwaona huko nyuma na wengine ataendelea kuwatazama kwenye mazoezi kuona ubora wao kupitia mechi hizo za kirafiki.
Miongoni mwa waliorejeshwa ni Banda anayekipiga Chippa United ya Afrika Kusini ambaye mara ya mwisho kuitwa katika kikosi hicho ni mwaka 2019.
Wachezaji wengine walioitwa ni Aishi Manula, Beno Kakolanya, Mzamiru Yassin na Habib Kyombo (Simba), Said Kipao, Datius Peter, David Luhende na Abdallah Mfuko (Kagera Sugar), Kibwana Shomari, Dickson Job na Feisal Salum (Yanga).
Abdulmalick Adam na Mohammed Banka (Namungo FC), Carlos Protas na Ibrahim Joshua (Tusker FC ya Kenya), Oscar Masai (Geita Gold), Himid Mao (Ghazl El Mahalla- Misri), Sospeter Bajana (Azam FC), David Uromi (Moroka Swallows-Afrika Kusini), Mbwana Samatta (Genk, Ubelgiji), Simon Msuva (Al Qadsiah FC- Saudi Arabia) na Said Khamis (Hatta Club-UAE).
Kimataifa Banda aitwa Stars, Mpole, Zimbwe waachwa
Banda aitwa Stars, Mpole, Zimbwe waachwa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
