Na mwandishi wetu
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, Yanga leo wameendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 huku mabao yote ya Yanga yakifungwa na Feisal Salum au Fei Toto.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na kutawaliwa na ushindani kwa timu zote, walikuwa ni Azam walioanza kuliona lango la Yanga katika dakika ya 25 ya mchezo huo kwa bao lililofungwa na Daniel Amoah, bao ambalo lilidumu kwa dakika 45 za kwanza.
Fei Toto aliwainua vitini mashabiki wa Yanga dakika 12 baada ya kuanza kipindi cha pili lakini furaha ya mashabiki wa Yanga ilidumu kwa dakika nane tu baada Ndoye Malickou kuipatia Azam bao la pili na kuwafanya ‘Wananchi’ waliofika Kwa Mkapa kuishuhudia timu yao kulazimika kuwa kimya wasiamini kilichoikuta timu yao.
Juhudi za Yanga kusaka bao la kusawazisha zilionekana kuzaa matunda katika dakika ya 67 baada ya Benard Morrison kufanyiwa madhambi na mwamuzi Ahmed Arajiga kuamuru ipigwe penalti lakini shuti lililopigwa na Djuma Shaban liliishia mikononi mwa kipa wa Azam, Ali Ahmada.
Kukosa penalti hiyo hakukuwakatisha tamaa Yanga na juhudi zao ziliwapatia bao katika dakika ya 77 mfungaji akiwa ni Fei Toto kwa mara nyingine kwa shuti kali akiwa nje kidogo ya eneo la 18.
Fei Toto ambaye katika mechi ya leo alianzia kwenye benchi, mabao yake yamekuwa muhimu kwa Yanga kuendeleza rekodi yake ya kutopoteza mchezo katika Ligi Kuu ya NBC tangu msimu uliopita, mashabiki Yanga wanaweza wasiifurahie sare ya leo lakini wana kila sababu ya kujifariji kwa kuendelea na rekodi yao ya kutopoteza mchezo katika ligi hiyo.
Soka Mabao ya Fei Toto yalinda rekodi Yanga
Mabao ya Fei Toto yalinda rekodi Yanga
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
