Na mwandishi wetu
Kikosi cha timu ya Simba kimetua salama leo Khartoum, Sudan tayari kwa mechi mbili za kirafiki huku benchi la ufundi likifafanua kuwa mechi hizo zitawasaidia kuwaweka sawa licha ya kuanza vizuri Ligi Kuu ya NBC.
Timu hiyo ilianza safari yake alfajiri ya kuamkia leo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JNIA, Dar es Salaam ikipitia Addis Ababa, Ethiopia.
Ikiwa huko, Simba itacheza mechi mbili dhidi Asante Kotoko ya Ghana na Al-Hilal ya Sudan waliotoa mwaliko wa mechi hizo.
Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally ameeleza kuwa benchi la ufundi chini ya kocha Zoran Maki limefurahia uwepo wa mechi hizo ili wajiweke sawa zaidi kwani wanaamini muunganiko wa kikosi chao bado haupo sawa.
“Kocha Maki na wasaidizi wake wamefurahia mechi hizi za kirafiki kwa sababu pamoja ya kwamba tumeanza ligi kwa ushindi lakini bado timu yetu haijakaa sawasawa na muda wa kukaa sawa haupo tena.
“Kwa hiyo tumepata hizi nafasi na uzuri wa mechi hizi za kirafiki unacheza kwa ‘ku-relax’ huogopi kukosea kwa sababu una muda mwingi wa kujifunza kupitia mechi hizi tofauti na mechi za mashindano kunakuwa na presha, umakini mkubwa hivyo hauna nafasi ya kukosea kwenye mashindano,” alisema Ally.
Timu hiyo iliyoondoka na wachezaji 19, wengine wakisalia kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kwa ajili ya mechi ya kuwania kufuzu michuano ya Chan dhidi ya Uganda, ilitarajia kuanza mazoezi yake jana Ijumaa jioni.
Mchezo wao wa kwanza dhidi ya Kotoko utapigwa kesho wakati ule wa Al-Hilal wakitarajia kucheza Agosti 31 kabla ya kurejea Dar es Salaam Septemba Mosi, mwaka huu kwa ajili ya mechi yao ya mwisho ya kirafiki dhidi ya AS Arta ya Djibouti.
“Hatuendi kule kutafuta kombe, tunakwenda kutengeneza timu yetu ili tukirejea tuwe imara zaidi na baada ya mechi yetu ya mwisho Dar es Salaam tutakuwa tayari tumeiva kwa mechi yetu ya ligi inayofuata dhidi ya KMC,” alisema Ally.
Simba imeanza vyema kwenye Ligi Kuu NBC msimu huu ikiwa inaongoza ligi baada ya ushindi wa mechi mbili, ikiwa na pointi sita sawa na Yanga na Singida Big Stars zinazoshika nafasi ya pili na tatu, wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Wekundu hao wataumana na KMC Septemba 7 kisha wataivaa Nyassa Big Bullets ya Malawi Septemba 9 mwaka huu kwenye mechi ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Soka Simba yatua salama Khartoum
Simba yatua salama Khartoum
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
