Barcelona, Hispania
Mshambuliaji wa Barcelona, Robert Lewandowski ameibiwa saa yenye thamani ya dola 71,000 sawa zaidi ya Sh 150 milioni za Kitanzania, wizi ambao inadaiwa umetokea wakati akielekea kwenye mazoezi ya timu hiyo Jumatano iliyopita.
Polisi hata hivyo walifanikiwa kufuatilia tukio hilo na hatimaye kumkamata mtu aliyehusika na wizi huo ambaye baada ya kukwapua saa hiyo aliichimbia chini katika eneo la karibu.
Lewandowski ambaye amesajiliwa na Barcelona msimu huu akitokea Bayern Munich kwa ada ya Euro 45 milioni alikuwa akipiga picha na mashabiki nje ya uwanja wa mazoezi wa timu hiyo lakini ghafla mwizi huyo alifungua kioo cha abiria na kukwapua saa hiyo ambapo Lewandowski kumfukuzia lakini alishindwa kumkamata kabla ya baadaye kukamatwa na polisi wa eneo hilo.
Hapo kabla, klabu ya Barcelona imewahi kuwa na tatizo la ulinzi na usalama katika eneo la kuingilia kwenye uwanja wao wa mazoezi kwa baadhi ya wachezaji wao kulalamikia vitendo vya watu ambao huwabughudhi kwa kuwavuta kwa lengo la kupiga picha za video kwa ajili ya mtandao wa TikTok.
Hata hivyo zipo habari kwamba uongozi wa klabu hiyo unalifanyia kazi tatizo hilo na uko mbioni kufanya mabadiliko katika mfumo wao wa ulinzi na usalama ili kuepusha matukio ya aina hiyo kutokea kwa siku zijazo.
Lewandowski ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Poland, alianza kuiwakilisha Barcelona kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu Hispania au La Liga wiki iliyopita dhidi ya Rayo Vallecano, mechi iliyoisha kwa sare ya bila kufungana na kesho anatarajia kucheza mechi yake ya pili ya ligi hiyo dhidi ya Real Sociedad.
Kimataifa Lewandowski aporwa saa ya mamilioni
Lewandowski aporwa saa ya mamilioni
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
