Na mwandishi wetu
Kuanza vibaya kwa Kagera Sugar ikiruhusu kufungwa mabao 2-1 na Azam, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Francis Baraza amefunguka akisema kuwa kuzubaa kwa mabeki wake ndiyo kumewagharimu.
Kagera ilipoteza mechi yao hiyo ya kwanza ya ligi msimu huu iliyopigwa jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Akizungumza na GreenSports, Baraza alisema kwamba walicheza vizuri na vijana wake walijituma kwa namna alivyowaelekeza ingawa walikuwa ugenini lakini walimudu presha hiyo ila kulitokea makosa ya mabeki ambayo yaliwatibulia kuondoka na pointi siku hiyo.
“Nashukuru tumemaliza vizuri mechi, ilikuwa ngumu, nzuri na vijana walifanya kazi kubwa, nawapongeza sana japo kiufundi ilikuwa ni kulala au kusinzia kidogo kwa mabeki wetu na kutupelekea kuadhibiwa.
“Washambuliaji walifanya kazi yao vizuri kama ilivyokuwa sehemu nyingine maana walitupa bao la kuongoza lakini tukashindwa kulilinda na sasa tunajipanga kwa ajili ya mechi zinazokuja naamini tutarekebisha makosa,” alisema Baraza.
Mshambuliaji wa Azam, Tepsie Evans aliyefunga bao na kutoa pasi ya bao kwenye mechi hiyo alisema haikuwa rahisi kuondoka na ushindi dhidi ya Kagera kwa namna walivyojipanga na wachezaji walionao lakini kubaki kwenye mipango ya kocha wao, Abdihamid Moallin kuliwasaidia kurejea mchezoni.
“Tunashukuru tumepata alama tatu lakini tumecheza na timu imara sana, imejiandaa, ina wachezaji wazoefu ambao wamefanya vizuri msimu uliopita, walitutangulia lakini tulikuwa makini na kufuata yale mwalimu ametufundisha na kupata tulichokipata, tumeondoka na pointi tatu lakini sio tulichokusudia kukipata kwa asilimia mia.
“Kuhusu upande wangu nashukuru kwa timu inavyonilea kisoka na kunipa nafasi japo wapo kaka zangu walionizidi, kwa hiyo na mimi najitahidi kila ninapopewa nafasi napenda kujitoa kwa asilimia mia nifanye vizuri na nashukuru nimekuwa na mwanzo mzuri msimu huu,” alisema Evans.
Soka Kocha Kagera Sugar alaumu mabeki
Kocha Kagera Sugar alaumu mabeki
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
