Na Hassan Kingu
Klabu ya Yanga imeingia kwenye awamu nyingine ya uongozi wa Rais Hersi Said lakini imejikuta ikimpoteza Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Senzo Mazingiza Mbatha raia wa Afrika Kusini baada ya ombi lake la kutaka kung’atuka kupitishwa na uongozi wa juu.
Senzo anaondoka akiwa na historia yake ndani ya soka la Tanzania kwa miaka takriban mitatu aliyodumu kwenye ardhi hii akihudumu Yanga na Simba SC.
Kiufupi Yanga imepoteza jembe kwelikweli katika kukua kwao kisoka hasa kwenye utawala na namna ya kuendesha klabu kwenye mfumo mpya wa kampuni, mfumo ambao ni mgeni kwa timu hizo mbili ambazo zimepania kutawala soka la Afrika kwa miaka ya usoni.
Kwa kipindi cha miaka miwili ambacho Senzo amekuwa akifanya kazi na Yanga, amekuwa muunganiko mkubwa wa namna ya mawasiliano kiutawala kutoka kwa ngazi ya juu mpaka kwa wafuasi wa timu hiyo kupitia waandishi wa habari na vyanzo vingine mbalimbali.
Nje ya yote hayo kuna taarifa mbalimbali zisizo rasmi kuhusu kuondoka kwake, ikihusishwa na kurejea kwa kiungo Mghana Yanga, Bernard Morrison kwani hata Simba alihusishwa kuihama baada ya kutua kwa mchezaji huyo aliyewahi kukipiga Orlando Pirates ya Afrika Kusini japo mwenyewe ameeleza kuwa amefanya hivyo akihitaji kuungana na familia yake aliyokaa nayo mbali kwa kipindi kirefu.
Hayo yote tunaweza kuyaweka kando kwa sasa, kwa namna nilivyomfahamu au kupata picha ya mbali kwa Senzo, namuona ni mtu mwenye weledi hasa katika namna ya kusuka mipango ya pesa kwa faida ya timu kupitia hata kwa vyanzo vidogo ilivyonavyo.
Kwa Senzo timu kunufaika, timu kujulikana, timu kuwa na ushindani wa kweli uwanjani na nidhamu vilikuwa miongoni mwa vitu ambavyo kwangu nilimuona ni mwenye kuvipa kipaumbele.
Ndiyo maana sikustaajabu kupata taarifa za yeye kuwaniwa akafanye kazi na Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA) kutokana na utendaji wake kazi wenye maono zaidi kupitia soka.
Mpira wa sasa unahitaji mno nguvu ya pesa kwa ajili ya maarifa mengi ya kiutawala soka kwa ukanda husika kwa ufasaha zaidi na Senzo analifahamu hilo kwa jicho la tatu lenye upana mno ndiyo maana alipokuwa Yanga mara kadhaa alisisitiza kwamba akiuona wingi wa mashabiki wa Yanga anaiona pesa, hili ni jambo ambalo kwa kipindi kirefu halijafanyiwa kazi kikamilifu si kwa Yanga tu bali hata mahasimu wao Simba.
Senzo hakuwa mtu wa kuegemea kwenye majigambo na tambo za porojo kama ilivyo kwa viongozi wengi tulionao kwenye soka leo, yeye anatazama namna nzuri ya kuongeza nguvu ya utawala na sio kebehi na majigambo.
Yawezekana tukakubali kuingia kwenye ubishi kuhusu hili lakini kwangu ukweli unabaki kuwa Senzo alikuwa mfano wa jemedari aliyekuja kutoa taswira pana ya soka la Afrika na duniani linatakaje na timu zinatakiwa kuheshimiwa na kujitambua kwa kiasi gani kutoka hapo zilipo.
Licha ya uwepo wa matajiri Ghalib Said Mohamed Yanga na uwepo wa Mohammed Dewji pale Simba lakini uwepo wa Senzo kwenye kiini cha utendaji kazi wa kila siku kwa timu hizi, umelinufaisha mno soka la Tanzania, japo kwa kiasi chake kidogo alichokitoa lakini bado kimebaki kuwa msaada kwa timu hizi.
Senzo amefanya kazi Simba na Yanga na ajabu amekuwa kiongozi wa tofauti aliyeamua kuondoka kwenye timu hizo bila kelele baada ya hapo na bila ya kufungashiwa virago lakini pia anakuwa mtendaji wa juu wa kwanza kufanya kazi katika klabu hizi mbili, tumezoea kuwaona wachezaji wakifanya hivyo lakini sina kumbukumbu za ofisa mtendaji wa ngazi ya juu kutoka Simba na kwenda Yanga.
Nachelea kusema ameondoka kwenye hizi timu akiwa bado anahitajika, hata kama kulikuwa na migongano mingine ya chinichini iliyopelekea haya yote lakini bado inatafsirika alisimama kwenye weledi kwa kuifanya kazi yake ipasavyo na mwisho anaondoka taasisi ikiwa inaelekea mahali pazuri na zaidi ya hilo hajaacha nyufa wala misuguano ya wazi yenye mrengo wa kuivuruga klabu.
Hapo baadaye labda muda unaweza kutuambia nini hasa kilichomuondoa kama ni misuguano ya ndani au la lakini hata kama hiyo ndiyo sababu basi Senzo amejua namna ya kuishughulikia hali hiyo kwa kuondoka katika namna isiyotoa dalili zozote za uwapo wa shari kwani hadi sasa wanaohisi kulikuwa na ugomvi wanaongozwa na hisia zao bila kuwa na uhakika wowote.
Senzo amekuja, ametazama, amefanya kazi na ameondoka kama miongoni mwa ‘ma-legend’ wa mabadiliko ndani ya klabu hizi kongwe na maarufu Afrika Mashariki na Kati baada ya kukaa zaidi ya miaka 80 katika uso wa soka ambalo halikuwa na mvuto kibiashara ya kisasa ya mpira wa miguu na sasa kazi kwao! Na ndio maana nasema bado mtu wa aina ya Senzo anahitajika katika klabu hizi.
Soka Senzo bado anahitajika Yanga
Senzo bado anahitajika Yanga
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
