Na mwandishi wetu
Azam FC inatarajia kucheza michezo mitatu ya kirafiki ikiwa nchini Misri na kama ikiwezekana watacheza mechi moja na Simba pia kwa ajili ya kuwaweka vizuri zaidi vijana wao.
Kocha Mkuu wa Azam, Abdihamid Moallin ameyasema hayo leo ikiwa ni siku ya kwanza ya mazoezi ya timu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa 2022/23 kabla ya keshokutwa kuelekea Misri kwa ajili ya kambi rasmi.
Simba yenyewe ilishatangulia nchini Misri tangu Julai 15 kwa ajili ya kambi huku ikitarajia kurejea nchini Agosti 5 siku tatu kabla ya tamasha la Simba Day litakalofanyika Agosti 8, mwaka huu.
“Vijana wamerejea kutoka mapumzikoni wako vizuri, tumeanza mazoezi yetu ya kwanza kwa vipindi viwili kwa kwenda gym na uwanjani. Hali yao ni nzuri kwa sababu wamerudi wakiwa katika afya stahiki.
“Tunapaswa kujiweka fiti zaidi, kurejesha mfumo na kuwa fiti tena kwa ajili ya msimu mpya, tunapaswa kuwaweka tayari na kuwaongezea baadhi ya vitu vya ufundi kwa kucheza mechi za kirafiki pia.
“Muhimu zaidi ni kuwaunganisha wachezaji wapya ndani ya timu, tutacheza mechi za kirafiki tukiwa Misri na tutacheza mechi kama tatu hivi. Tunajua Simba wako kule na kama kutakuwa na nafasi ya kucheza nao basi tutafanya hivyo,” alisema Moalin.
Kocha huyo alifafanua kuwa kucheza na timu kutoka Ligi Kuu Bara itawasaidia wachezaji wao wapya kupata ladha ya ushindani wanaokwenda kukutana nao lakini pia timu kupata ushindani wa miongoni mwa timu watakazopambana nazo msimu ujao.
Soka Azam yaitaka Simba Misri
Azam yaitaka Simba Misri
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
