Na mwandishi wetu
Nyota ya mchezaji wa Simba Pape Sakho imeendelea kung’ara baada ya bao lake kuingia kwenye hatua ya mwisho ya tatu bora kuwania kipengele cha Tuzo ya Bao Bora la Mwaka kwenye tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Awali, bao la Sakho lilikuwa likishindanishwa na mabao ya wachezaji wengine tisa wanaoaminika kufunga mabao mazuri msimu huu kupitia ngazi mbalimbali zilizozikutanisha timu za Afrika kabla ya baadaye kufanyika mchujo na kubaki matatu.
Sakho raia wa Senegal alifunga bao hilo kwa ‘tik-taka’ dhidi ya Asec Mimosas walipokutana Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na Simba kushinda kwa mabao 3-1.
Bao jingine linaloshindania tuzo hiyo ni la Mmalawi Gabadinho Mhango wa Orlando Pirates alipoifunga Morocco bao la umbali wa mita 40 kwenye mechi za michuano ya Afcon 2021.
Mpinzani mwingine wa Sakho ni Mmoroco, Zouhair El Mountaraji wa Wydad Casablanca aliyefunga bao nje ya 18 kwenye fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo kubwa zaidi kwa ngazi ya soka Afrika inatarajiwa kufanyika kesho katika jiji la Rabat, Morocco.
Soka Bao la Sakho lazidi kupaa CAF
Bao la Sakho lazidi kupaa CAF
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
