Na mwandishi wetu Wakati mchezaji nyota mpya wa Simba, Moses Phiri akitarajiwa kujiunga na timu hiyo kesho, imeelezwa pia mazoezi ya Wekundu hao yameanza nchini Misri kwa mzuka wa aina yake.
Simba iliondoka nchini juzi Alhamisi na kufika alfajiri ya kuamkia Ijumaa ambapo jioni yake wakaanza mazoezi yao ya kwanza chini ya kocha wao mpya, Zoran Maki.
Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally ameeleza kwamba mazoezi hayo wameanza kufanya kwenye hoteli ya kifahari waliyofikia jijini Ismailia nchini humo.
Amesema kurejea kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi, Jonas Mkude, Clatous Chama na Shomari Kapombe kumeibua ari mpya katika mazoezi hayo ya maandalizi ya msimu mpya wa 2022-23 unaotarajia kuanza mapema mwezi ujao.
“Wachezaji wote wako timamu, tumeanza rasmi mazoezi na kocha Maki na niseme kwamba mazoezi yamekwenda vizuri sana, tunamshukuru Mungu wale wachezaji ambao walimaliza msimu wakiwa na majeraha kuanzia Mkude, Chama na Kapombe wamefanya mazoezi na hali ni safi kabisa.
“Wapo wachezaji ambao hawajajiunga nasi huku kama Phiri, Nasoro Kapama ambao taratibu mbalimbali zinaendelea na mpaka ikifika Jumapili (kesho) nyota hao watakuwa washajiunga na wenzao na maandalizi yataendelea tukiwa tumekamilika,” alisema Ally.
Ally pia alibainisha kuwa baada ya timu kukaa sawa kwenye program za sasa za kujenga utimamu wa mwili na kutengeneza muunganiko wa kikosi, watacheza mechi za kirafiki takriban tatu ambapo baadaye watataja watacheza na nani na ratiba nzima ya michezo hiyo.
Simba ambayo imepoteza makombe yake ya Ligi Kuu Bara na FA kwenye msimu uliomalizika hivi karibuni inatarajia kurejea nchini Agosti 5 kwa ajili ya tamasha lake la Simba Day siku tatu baadaye kisha itapepetana na Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii mnano Agosti 13, mwaka huu.
Soka Mazoezi ya Simba Misri yanoga
Mazoezi ya Simba Misri yanoga
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
