Na mwandishi wetu
Uvumi kuhusu mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele kujiunga na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini umepamba moto mitandaoni, hata hivyo mshambuliaji huyo ameweka kando uvumi huo badala yake ametumia muda huu kumpongeza mfungaji bora wa msimu huu, George Mpole wa Geita Gold aliyepachika mabao 17.
Pongezi hizo ni baada ya wawili hao kukimbizana takriban msimu mzima wakichuana kufunga mabao, mchuano uliokwenda mpaka kwenye mechi za mwisho za Ligi Kuu ya NBC zilizomalizika jana.
“Nichukue nafasi hii kutoka ndani ya moyo wangu kukupongeza kwa jitihada zako kufanikiwa kuwa mfungaji bora kwa kufunga mabao 17 katika msimu wa 2021/22, nakutakia kila la heri,” alieleza Mpole kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.
Kabla ya mechi za jana, Mayele raia wa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo alikuwa amefungana kwa mabao 16 na Mpole lakini akashindwa kufunga kwenye mechi yao waliyoshinda bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar wakati Mpole akitingisha nyavu kwenye sare ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union.
Mayele ambaye amekuwa mchezaji muhimu wa Yanga msimu ulioisha jana anatarajiwa kuendelea kuibeba timu hiyo katika michuano ya klabu Afrika na Ligi Kuu msimu ujao, kwa sasa anahusishwa na mipango ya kuihama klabu hiyo akidaiwa kuelekea Afrika Kusini habari ambazo hata hivyo bado hazijathibitishwa.
Katika mbio za ufungaji mabao, huu unakuwa msimu wa pili mfululizo kwa mchezaji wa Tanzania kuwa mfungaji bora wa ligi baada ya John Bocco anayekipiga Simba kufanya hivyo msimu uliopita akifunga mabao 16.
Misimu miwili nyuma kabla ya Bocco, Meddie Kagere wa Simba raia wa Rwanda alitwaa kiatu cha ufungaji bora mara mbili mfululizo baada ya msimu wa 2018-19 kufunga mabao 23 na msimu uliofuata akatikisa nyavu mara 22.
Soka Mayele ampongeza Mpole
Mayele ampongeza Mpole
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
