Jonathan Haule
Simba imemaliza msimu wa 2021/22 bila taji la Ligi Kuu Bara, hiyo ni baada ya kulibeba taji hilo kwa misimu minne mfululizo, mara tu baada ya kupoteza matumaini ya kulitetea taji, tafrani za hapa na pale zikaanza kuibuka.
Uvumi wa timua timua ukaanza kusikika, ikaonekana kuna watu wanaotakiwa kutimuliwa, mmoja wa watu ambaye tayari ameshakumbana na timua timua hiyo ni aliyekuwa kocha mkuu, Pablo Franco kutoka Hispania, yeye na baadhi ya wasaidizi wake wameshatimuliwa na timu sasa ipo chini ya kocha msaidizi, Suleiman Matola.
Ukiachana na Pablo, mwingine aliyeanza kutajwatajwa katika timua timua hiyo ni mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez, huyu pamoja na kupewa sifa zote hapo kabla naye akatajwa kuwa ni tatizo ingawa alikuwa imara na baadhi ya wanasimba kumtetea hivyo jaribio baya ambalo halikuwa na mantiki dhidi yake likagonga mwamba.
Matukio yote hayo mawili kwangu nayafananisha na hadithi ya kumsaka bundi anayeonekana, unajua tatizo lakini badala ya kutulia na kutafuta suluhisho unatumia kushindwa kulibeba taji la ligi kama kigezo cha kukuza tatizo na kufanya ionekane kama wasemwavyo waswahili kwamba bundi kawavamia yaani klabu ya Simba imevamiwa na bundi hivyo ni lazima asakwe.
Simba ina matatizo madogo tu ya viongozi kukaa chini na kuyaweka sawa, hakuna sababu ya kutumia nguvu nyingi kutimuana na kugombana nyinyi kwa nyinyi wakati mkitulia suluhisho linaonekana.
Simba ambayo imelikosa taji la Ligi Kuu Bara inashika nafasi ya pili katika ligi hiyo hiyo na itamaliza katika nafasi hiyo hiyo, imetoka katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kutolewa katika hatua ya robo fainali na Simba hao hao ndio vinara wa Ngao ya Jamii.
Mazingira au matokeo ya aina hiyo si ya kuanza kushikana uchawi, bali ni ya kukaa chini na kuangalia nini cha kufanya ili kusonga mbele lakini inapotokea watu wakaanza kusaka wachawi au bundi maana yake ni kwamba wanalazimisha au wanatengeneza mitafaruku ambayo badala ya kwenda mbele inaweza kuwa sababu ya kurudi nyuma.
Kutawala ligi miaka minne si jambo rahisi, ni jambo la kupongezwa na ingawa kulikosa kunauma lakini katika kutafuta namna ya kulirudisha taji hilo umakini unahitajika vinginevyo hali itazidi kuwa mbaya, badala ya kumaliza ligi nafasi ya pili kama ilivyotokea msimu huu, msimu ujao timu itamaliza nafasi ya nne au tano, na katika michuano ya Afrika itakuwa ya kuingia na kutoka raundi ya kwanza.
Simba inachotakiwa kufanya ni kuimarisha kikosi, kusajili wachezaji wa kuleta nguvu na ari mpya, kuna aina ya mchoko wa wachezaji ulioonekana katika klabu hiyo au kubweteka na hilo linaweza kuwa limechangiwa na mengi lakini inaweza kuwa moja ni mafanikio ya miaka minne niliyoyataja hapo juu.
Na hili ni jambo la kawaida kwa binadamu tulio wengi tunapopata mafanikio tena wakati mwingine mafanikio madogo tu kwa mwaka mmoja au miwili mfululizo kuna hali ya kubweteka, kuridhika na kujiona uko juu au kuwa katika mchoko, sasa fikiria hali inakuwaje kwa aliyefanikisha jambo lake kwa miaka minne mfululizo.
Kwa hali hiyo kinachotakiwa kwa Simba ni kwa benchi la ufundi kuwa makini na usajili, tayari tumeona maingizo mapya katika Simba, mmoja akiwa ni Moses Phiri kutoka Zambia, na wengine wakianza kuachwa, hilo ndilo jambo la kulipa nafasi yake kwa kipindi hiki ili kujiandaa na msimu ujao.
Wachezaji wa Simba ambao wameitumikia timu hiyo katika misimu mitatu au minne ya mafanikio kwa kuwaangalia haraka haraka wengi wao umri ni kuanzia miaka 30 na kuendelea, si miaka 40 lakini siwezi kushangaa siku akitokea mtu akiniambia wako wenye umri huo.
Kwa hiyo usajili makini wa kupunguza mchoko utakaoondoa hali ya kubweteka ndio suluhisho namba moja, haya mengine ya kufukuzana na kulazimisha shari yasipewe nafasi.
Hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii kulikuwa na hali ya kucharurana na kufanyiana dhihaka kwa mashabiki wa Simba na Yanga baada ya Yanga kutwaa taji, katika mjadala mmoja nilioufuatlia shabiki mmoja ambaye naamini atakuwa wa Simba yeye alikuja na maneno machache yaliyonifurahisha.
Kwanza aliwapongeza Yanga akawaambia anajua raha ya ubingwa na kuwataka watafakari hali ya furaha waliyonayo sasa na jinsi ilivyokuwa kwa Simba kwa miaka minne mfululizo. Nafikiri baada ya kulikosa taji Simba wawe na mtazamo kama wa huyu shabiki badala ya kufikiria kumsaka bundi anayeonekana.
Soka Uchovu, kubweteka vimeiathiri Simba
Uchovu, kubweteka vimeiathiri Simba
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
