Na Jonathan Haule
Katika usajili wa kiungo wa Asec Mimosas ya Ivory Coast, Stephane Aziz K, Yanga inatakiwa kuuambia umma jambo moja kati ya mawili, ni ama imemkosa mchezaji huyo au mazungumzo bado yanaendelea. Kwa sasa iachane kidogo na hadithi ya tumeshamsajili.
Najua kama itatokea mpango wa kumsajili mchezaji huyo umefeli kuna ugumu kidogo kuuambia umma jambo hilo, na hiyo ni kutokana na habari zake kupamba moto kwenye mitandao ya kijamii, habari ambazo ziliambatana na picha na hivyo kuwaaminisha baadhi ya mashabiki kwamba kila kitu tayari.
Katika hali ya kawaida, picha pekee haitoshi kumuaminisha mtu kwamba umemsajili mchezaji badala yake maandishi yaliyosainiwa na pande zote mbili au pande zote kukiri kwamba zimefikia makubaliano, bahati mbaya sana kinachoonekana ni kama vile kuna ugumu wa hilo kufanyika jambo ambalo linatoa ishara kwamba ni ama mazungumzo hayajakamilika au usajili umefeli.
Hoja na mijadala ya kwenye mitandao ya kijamii hasa zile hoja zinazotolewa na watu wanaoonekana kuwa wanazi wa Yanga ni kwamba mchezaji huyo tayari ni wa Yanga na kwa wale wasio wa Yanga wako wanaopinga kishabiki lakini kuna ambao hawapingi badala yake wanataka ushahidi iwe wa maandishi au hata kauli za pande zote mbili na si picha pekee kwamba Aziz K amesajiliwa Yanga.
Simba majuzi wamemsajili Moses Phiri kutoka Zambia, habari ile haikuishia kwa Simba tu kusema au kutuma picha zake mitandaoni, bali kwa mchezaji mwenyewe kukiri, imekuwa hivyo kwa wachezaji wengi, kwa Aziz K ni ama kuna siku itakuwa hivyo au imeshindikana.
Kwa wanaochambua mambo kwa kina tayari wanahisi huenda mpango mzima wa usajili wa mchezaji huyo umefeli, hilo unaweza kuliona ukifuatilia hoja za mitandaoni, anayehoji uthibitisho kwamba mchezaji huyo kasajiliwa Yanga hakuna anayekuwa tayari kumthibitishia au kumpa uthibitisho wowote zaidi ya picha au ataambiwa athibitishe yeye kama mchezaji huyo hajasajiliwa Yanga au anaweza hata kujikuta akitukanwa na kuambiwa kwamba kauli zake zinatokana na chuki dhidi ya Yanga.
Naomba uthibitisho, badala ya kunipa uthibitisho unanitukana au unaniambia mimi ndio nithibitishe, ni kama vile mtu anakwambia amenunua gari jipya ukimwambia nionyeshe uthibitisho wa hilo gari, anakwambia uthibitishe wewe uliyehoji kuhusu yeye kununua gari jipya.
Ukiniuliza msimamo wangu kuhusu usajili wa Aziz Ki kwenda Yanga, nitakwambia niko 50-50, siwezi kukuhakikishia kwamba mchezaji ni wa Yanga kwa sababu wenyewe hawajathibitisha lakini pia huenda mazungumzo yanaendelea lakini pia huenda mazungumzo yamefeli, kwangu ushahidi wa picha pekee hautoshi kuniambia kwamba tayari ni mchezaji wa Yanga.
Ndio maana nasema Yanga wanatakiwa kusema mambo mawili tu ni ama mazungumzo yanaendelea au wameshindwa kumpata mchezaji huyo lakini si kuja na ushahidi wa picha.
Kwanza katika zama hizi picha pekee haitoshi kuwa uthibitisho wa jambo, picha hiyo hiyo ikifika mikononi mwa wataalam wasio na maadili inaweza kuchezewa na hatimaye kuufanya uwongo uonekane ukweli na ukweli uonekane uwongo.
Miaka ya nyuma ambayo walau kidogo ushahidi wa picha ulikuwa na maana bado kuna wakati haukutosha kuwa uthibitisho pekee, tuliwahi kushuhudia mchezaji Ephraim Makoye akisajiliwa Simba na picha zikapigwa akiwa na viongozi wa Simba katika tukio hilo lakini mwisho wa siku Yanga wakadai mchezaji huyo huyo ni wao, walimsajili na wakampata.
Nasisitiza, badala ya picha Yanga wajitokeze hadharani waseme ama mazungumzo yanaendelea au wamemkosa Aziz K, najua hili la kumkosa kama kweli wamemkosa linaweza kuwa gumu kwao lakini ugumu wameutengeneza wenyewe na zaidi ya hilo hawana sababu ya kuona ugumu kwani Yanga si klabu ya kwanza kumkosa mchezaji iliyemtaka kwa kuzidiwa ujanja na mpinzani wa ndani au wa nje.
Tukumbuke namna ambavyo Chelsea wakati huo ikinolewa na Jose Mourinho ilivyowazidi ujanja Man United na kumsajili John Obi Mikel kutoka klabu ya Lyn ya Norway wakati Man United wakiwa tayari wamefanya mazungumzo ya awali na kujiaminisha kwamba watampata mchezaji huyo.
Tukio la Mikel nalo liliambatana na upigaji picha tena si picha ya ndugu zake bali ni picha ya Mikel mwenyewe akiwa amevaa jezi namba 21 ya Man United, na japo usajili huo uliambatana na matukio mengi zikiwamo habari zisizo rasmi kwamba Mikel alitekwa lakini mwisho wa siku picha haikuwasaidia Man United kumfanya Mikel awe mchezaji wao.
Katika hilo mifano ni mingi lakini ikumbukwe pia kwamba hakuna mchezaji anayejielewa wa Afrika apate timu Ulaya, iwe hata Ulaya Mashariki na akaamini hiyo kwake baadaye inaweza kuwa njia ya kuelekea Ufaransa, England au Hispania halafu akakataa kwa ajili ya Yanga au Simba.
Inawezekana hata kwa Aziz K hali ni hiyo, amechagua timu nyingine kwa sababu ameifikiria kesho yake na amejiwekea malengo makubwa au pia inawezekana kuna timu imemtangazia dau kubwa kuliko la Yanga, yote hayo yanawezekana na ni mambo ya kawaida, Yanga waseme wasione tabu.
Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair wakati nchi yake imeivamia Iraq kwa madai kwamba Rais wa nchi hiyo Saddam Hussein alikuwa na silaha za maangamizi lakini baada ya kuingia katika nchi hiyo na kufanya upekuzi silaha hizo hazikuonekana licha ya kuuaminisha Ulimwengu wote kwamba kiongozi huyo alikuwa na silaha za maangamizi, hivyo Blair na washirika wake wakasakamwa na makundi mbalimbali duniani.
Siku moja Blair katika kujibu hoja hiyo alisema. “Tunajua tulisema Saddam Hussein ana silaha za maangamizi na tunajua hatukuziona.”
Natarajia Yanga nao waibuke na kusema. “Tunajua tulisema tumemsajili Aziz K na tunajua tumeshindwa kumpata.” Lakini pia wanaweza kusema. “Tunajua tumezungumzia usajili wa Aziz K na kwa sasa mazungumzo ya usajili bado yanaendelea.
Soka Yanga iseme moja kuhusu Aziz K
Yanga iseme moja kuhusu Aziz K
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
