Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele ana mabao 16 lakini amekiri kupata changamoto na ushindani mkubwa kwa George Mpole wa Geita wanayechuana katika mbio za kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya NBC Bara.
Mayele ambaye ni raia wa DR Congo juzi alifunga mabao mawili na kutoa asisti moja kwenye ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union na kumpiku Mpole mwenye mabao 15.
Kwa muda mrefu wawili hao wamekuwa wakichuana kukiwania kiatu cha ufungaji bora ambapo Mayele emeeleza kuwa kwa namna wanavyoshindana ni wazi kila mmoja amekuwa akimsukuma mwenzake kujituma na anaamini hiyo imewasaidia mno kufika walipo sasa.
“Mechi tatu zimebaki nitaendelea kupambana nifanye vizuri pia kwenye mechi hizo na nimalize vizuri. Yule (Mpole) anatoa mchango kwa timu yake na mimi natoa kwa timu yangu na imepelekea kuwa ni ushindani mkubwa. “Yeye akifunga na mimi nasema moyoni kwamba itabidi nifunge na ninaamini hata yeye pia atakuwa anasema hivyo hivyo huko kwamba atafunga mechi ijayo, naamini tutashindana hivi mpaka mwisho,” alisema Mayele.
Kuhusiana na kuisaidia timu hiyo kuchukua taji la Ligi Kuu ukiwa ni msimu wake wa kwanza kukipiga Yanga alisema: “Kwanza nashukuru kwa huu ubingwa, tumetimiza lengo la kwanza la msimu huu, nawashukuru wote waliosababisha hili kwa kweli.
“Lakini ilikuwa ngumu kwa kweli kwangu maana ndiyo msimu wa kwanza nakuja hapa, nilimuomba Mungu katika hilo nashukuru mpaka leo kufanikisha hili imekuwa furaha kwangu na niwashukuru tena wote tuliokuwa pamoja kulifanikisha hili.”
Soka Mayele akiri Mpole mshindani
Mayele akiri Mpole mshindani
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
