London, England
Mshambuliaji wa Tottenham na timu ya Taifa ya England, Harry Kane amesema ujio wa Erling Haaland na Darwin Nunez katika Ligi Kuu England (EPL) ni changamoto nzuri itakayomfanya awe bora zaidi msimu ujao.
Kane ambaye kwa sasa anaiwakilisha timu ya Taifa England katika Uefa Nations League, ametoa kauli hiyo ikiwa ni saa kadhaa baada ya Man City kukamilisha usajili wa Haaland kutoka Borussia Dortmund ya Ujerumani na Liverpool kukamilisha usajili wa Darwin Nunez kutoka Benfica ya Ureno.
Kane alikuwa akihusishwa mara kadhaa na mipango ya kuondoka Tottenham na kujiunga na Man City lakini mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy alikuja na ofa ya juu akitaka kumuuza mchezaji huyo kwa kiasi cha Pauni 150 milioni, dau ambalo kocha wa City, Pep Guardiola hakuwa tayari kulikubali.
Kane mwenye miaka 28 sasa na ambaye amewahi kutwaa kiatu cha dhahabu mara tatu katika miaka saba iliyopita, anatarajia kuendelea kuwa katika kikosi cha timu hiyo hasa wakati huu ambao kocha Antonio Conte anadaiwa kuwa na mikakati kabambe ya kuifanya timu hiyo iwe ya kutoa ushindani katika kulisaka taji la EPL.
Alipoulizwa iwapo ujio wa Haaland na Nunez katika EPL utatishia nafasi yake katika kuwa mfungaji bora, Kane ambaye msimu ulioisha wa 2021/22 alishika nafasi ya pili nyuma ya Mohamed Salah wa Liverpool na mchezaji mwenzake wa Tottenham Heung-Min Son waliokuwa na mabao 23 kila mmoja, alisema kwamba mbio za kuwania kiatu cha dhahabu wakati wote ni ngumu.
“Kwa miaka kadhaa sasa Ligi Kuu England imekuwa ikitoa washambuliaji wenye uwezo wa juu duniani kote, unatarajia kila mshambuliaji wa kiwango cha juu atake kucheza Ligi kuu England na usajili wa hao wawili ndio hali halisi, inasaidia, itanisaidia mimi kukua kama mchezaji, kunapokuwa na ushindani mzuri inanifanya kujibidiisha zaidi na kuwa bora, kwa hiyo naisubiri changamoto hiyo,” alisema Kane.
“Kwanza nitajaribu kujiangalia mimi, ninapoingia katika msimu wowote ninakuwa na mambo ninayotaka kuyafanikisha na malengo ninayotaka kuyafikia, katika hilo najitahidi sana nisiwe mwenye kuwaangalia wachezaji wengine,” aliongeza Kane ambaye kesho anatarajia kuiwakilisha England katika mechi dhidi ya Hungary.
Kimataifa Kane awafurahia Nunez, Haaland EPL
Kane awafurahia Nunez, Haaland EPL
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
