Madenge akabidhiwa Biashara United
Na mwandishi wetu
Baada ya timu ya Biashara United juzi kulivunja benchi la ufundi la timu hiyo lililokuwa chini ya kocha mkuu, Vivier Bahati mapema imemkabidhi majukumu ya kukinoa kikosi hicho, mkurugenzi wao wa ufundi, Omary Madenge.
Timu hiyo ilimuondoa Vivier kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo inayowania isishuke daraja na sasa imejinasibu kuwa itahakikisha inapambana kufanya vizuri kwenye mechi nne zilizosalia.
Biashara kwa sasa inashikilia nafasi ya 15 kwa pointi 24, sawa na Mbeya Kwanza inayoburuza mkia huku ikizidiwa pointi moja na Tanzania Prisons inayoshikilia nafasi ya 14.
“Bado tunapambana hivyo lazima tuendelee na mazoezi, bado mechi nne muhimu sana kwenye mustakabali wa timu yetu, tutafanya vizuri na bahati nzuri vijana wote nawafahamu, kwa hiyo wapo chini yangu na tutafanya kile Wanamara wanakihitaji ili tunusurike kwenye hatari tuliyopo,” alisema Madenge.
Katika mechi hizo nne, Biashara inatarajia kuumana na Kagera Sugar na Geita Gold ugenini kisha itakipiga na KMC ikiwa nyumbani kabla ya kutua Dar es Salaam kumalizana na Azam FC.
Mwisho.
