Jonathan Haule
Wengi wetu tumewahi kuwasikia baadhi ya wapenzi au wanandoa wakijadiliana kuhusu suala zima la uzazi wa mpango.
Walio wengi wanapenda au wanaamini katika uzazi wa mpango lakini njia ipi sahihi ya kuitumia katika hilo ni kitu ambacho kimekuwa kikiwatatiza.
Wako ambao tayari wanatumia madawa, wako ambao hudiriki kutoa mimba na wako ambao huzaa bila mpango lakini wangependa wazae watoto kwa kuzingatia uzazi wa mpango kwa kuwa ni jambo lenye faida kubwa kwa afya ya mama na ustawi wa familia.
Njia ambayo imekuwa ikihubiriwa na kunadiwa na watu mbalimbali kwa madai kwamba ndio njia sahihi katika uzazi wa mpango ni utumiaji wa madawa lakini hapo hapo kuna kundi kubwa linaloiogopa njia hiyo kwa madai kwamba ina madhara au si salama na wengine hudiri kusema kwamba haifai.
Yapo madai mengi dhidi ya madawa haya, wapo wanaodai kwamba huwafanya baadhi ya wanawake kunenepa, wengine wanadai unaweza kupata mtoto mmoja halafu usipate tena, wapo pia wanaodai kwamba madawa haya huharibu mfumo mzima wa mwanamke katika siku zake za kila mwezi na wengine huyahusisha na magonjwa mbalimbali.
Si nia yangu kujadili kufaa au kutofaa kwa njia hii lakini kwa kuwa kuna kundi kubwa linaloiogopa njia hii na haliko tayari kuitumia na hapo hapo wanapenda kuzaa kwa kuzingatia uzazi wa mpango, ningependa tu kuweka bayana kwamba inawezekana kupanga uzazi bila kutumia madawa, hivyo kwa wenye hofu ya utumiaji madawa nao wanaweza kabisa kupanga uzazi.
Katika kupanga uzazi bila kutumia madawa kwanza kabisa ni vyema kutambua siku zako za kupata ujauzito na siku ambazo huwezi kupata ujauzito au hakuna uzazi.
Katika hili ni vyema mwanamke na mwanaume wakashirikiana lakini kwa kuwa mwanamke ndiye anayebeba mimba ni vyema akawa kiongozi wa jambo hili.
Na hapa ningependa tu kuweka wazi kuwa kama una tatizo la kuzijua siku hizo usipate tabu mtafute daktari yeyote aliyebobea katika eneo hilo atakufahamisha vizuri kama kuna ugumu wa kumpata daktari au mtaalam wa afya hata manesi, wakunga na wahudumu wengine wa afya wako makini katika suala hili, jambo la muhimu ni kutafuta mtu sahihi.
Kumbuka kwamba siri kubwa ya uzazi wa mpango bila kutumia madawa imejificha katika kuzitambua siku zako zilizo salama na zisizo salama, bila hivyo hutoweza kupanga uzazi badala yake utahitaji kutumia madawa au kuendelea kuzaa bila kufuata uzazi wa mpango.
Kwa kuzijua siku zako utakuwa umefanya jambo muhimu la kwanza katika utaratibu mzima wa uzazi wa mpango bila kutumia madawa, baada ya hapo kuna mambo ya kawaida ya kuyazingatia.
Kwanza kabisa ni kujiongeza wewe mwenyewe na mpenzi wako, kwa mfano kama daktari/mtaalam/ amekwambia siku salama kwa maana hakuna uzazi zinaanzia tarehe 14, 15, 16, 17, 18 na kuishia 19, jizuie kufanya tendo la ndoa tarehe 14 na 19, anza 15 hadi 18.
Siku ya 19 pia ni muhimu kujizuia kwani inaweza kuwa na uzazi kutokana na mabadiliko ya siku kwa kila binadamu hivyo hadi hapo kwa mwezi utakuwa na siku nne za kufanya tendo la ndoa bila kupata ujauzito.
Nimetolea mfano wa siku nne lakini zinaweza kuwa zaidi ya hizo kutokana na maelekezo ya mtaalam wa uzazi kwa jinsi atakavyokutajia idadi ya siku za kupata ujauzito na kutopata ujauzito.
Kumbuka tu jambo la muhimu hapo ni kujiongeza yaani kuongeza siku moja ya kuanza na kupunguza siku moja ya kumaliza, lengo likiwa ni kujihami na mabadiliko yoyote yanayoweza kutokea katika siku zako.
Siku nne za kufanya tendo la ndoa kwa mwezi si chache, zinatosha kabisa kuimarisha uhusiano na zinaweza kuwa hata 10 kwa mwezi kwa namna ambavyo mtaalam atakutajia siku gani uzazi haupo na siku gani uzazi upo lakini la muhimu ni kuchelewa siku moja au hata mbili za kuanza tendo na kuacha siku moja au mbili kabla ya kuingia katika siku ambazo uzazi upo.
Hapo hapo kuna ukweli kwamba hata kama siku zisizo na uzazi zitakuwa 10 au hata zaidi, natambua ukweli kwamba binadamu tumeumbwa na tamaa, tuna matamanio inaweza ikatokea siku ambazo hazina uzazi zimepita na matamanio ya tendo la ndoa yamekujia katika siku ambayo uzaziupo.
Matamanio au tamaa hizi huwatesa zaidi wanaume, anapokuwa na hamu na tendo inakuwa vigumu kujizuia hasa mpenzi wake akiwa karibu, kibaya zaidi wapo baadhi ya wanaume ambao hudiriki kuwa wakali kwa wapenzi wao pindi wanapohitaji tendo la ndoa.
Mwanamke atajaribu kujizuia lakini mwanaume anakuwa mbishi na kujikuta wote wanaingia katika kufanya tendo na baada ya hapo mwanaume anaanza kujiuliza au hata kujilaumu kwamba ni kwanini asingesubiri siku ambazo hakuna uzazi.
Zipo njia kadhaa za kujizuia na matamanio haya, njia ambazo ni muhimu zikafanywa na mwanaume na mwanamke kwa kushirikiana ingawa mwanamke ambaye ndiye mbeba ujauzito anatakiwa kuwa mstari wa mbele.
Kwa kuwa inashauriwa kupata ujauzito baada ya mtoto wa mwisho kufikisha miaka zaidi ya miwili au mitatu, mtoto mdogo uliyenaye anaweza kukusaidia katika kujizuia na matamanio au kuwafanya msifanye tendo la ndoa.
Lala na mtoto wako halafu hakikisha unamkumbatia ili kuzuia baba kukusogelea, lakini kama hilo ni gumu chelewa kulala, mume akionyesha dalili za kutaka tendo la ndoa katika siku yenye uzazi usiingie chumbani mapema au usilale mapema, washa televisheni, soma kitabu au tafuta jambo lolote la kukushughulisha ili tu mwenza wako apitiwe na usingizi.
Kumbuka kwamba siku unayoishindania ni moja, ukifanikiwa leo utakuwa umefanya jambo kubwa hivyo usione tabu kufanya hivyo hivyo kesho na hapo utakuwa umefanikiwa katika siku nyingine moja. Utaona siku zinapita hadi kuifikia siku ambayo hakuna uzazi na hapo utakuwa huru kufurahia tendo la ndoa.
Jambo hili japo linatakiwa zaidi kufanywa na mama ambaye anazuia ushawishi wa baba, lakini baba naye akijiona katika hali ya kutaka kufanya tendo siku ambayo kuna uzazi si vibaya akatafuta jambo la kumshughulisha kama kusoma kitabu, kuangalia televisheni.
Katika kusoma vitabu hapa unaweza pia kusoma vitabu vya dini, muislamu au mkristo chukua Kuran au Biblia, isome kwa kutafuta Baraka za Mungu wako lakini pia isome kwa kutafuta maarifa kwani vitabu hivi ukivisoma na kuvielewa vizuri vina mengi ya kusisimua na vitakupa maarifa mengi mapya.
Baba au hata mama pia anaweza kufanya jambo lolote litakalomfanya baada ya muda mfupi kujisikia usingizi mzitona hatimaye kuamua kulala bila kufanya tendo la ndoa, anaweza kusoma kitabu, kutafakari namna maisha yake yanavyokwenda nini afanye kuboresha kazi aifanyayo au kusaka mafanikio katika kazi yake.
Pia ikiwezekana fanya mazoezi ya jioni, hili pia ni jambo muhimu linaloweza kukusaidia kupanga uzazi bila kutumia madawa lakini ni muhimu kuhakikisha unafanya mazoezi yatakayouchosha mwili na kukufanya baada ya hapo akili yako ifikirie kula, kunywa na kupumzika kwa maana ya kulala.
Katika hili ni lazima niwe muwazi kuwa mazoezi mepesi na ya muda mfupi yanaweza yasiwe na msaada badala yake yanaweza kukuhamasisha kupata hamu ya kufanya tendo la ndoa, fanya mazoezi ya kutosha yatakayouchosha mwili.
Tukutane tena juma lijalo
