London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema ataendelea kusajili wachezaji ili kukifanya kikosi chake kiwe bora baada ya kumkosa Vinicius Junior ‘Vini Jr’ aliyekubali kuongeza mkataba Real Madrid.
Baada ya kuwapo uvumi kuhusu Arsenal kumsajili Vini Jr kutoka Real Madrid, hali ilibadilika kwa mchezaji huyo kukubali ofa nono ya miaka sita na sasa Arsenal wameamua kuhamishia nguvu zao kwingineko.
Arteta aliulizwa na waandishi wa habari baada ya mechi ya kirafiki dhidi ya Borussia Dortmund Jumapili iliyopita iwapo mashabiki watarajie ongezeko la wachezaji, kocha huyo alisema hicho ndicho wanachotaka kukifanya.
“Ni lazima awe mchezaji sahihi katika soko ili kukifanya kikosi chetu kiwe bora zaidi, tunaliangalia hilo kwa sasa,” alisema Arteta.
Kabla ya Arsenal kufungwa mabao 3-2 na Borussia Dortmund kwenye Uwanja wa Emirates, siku hiyo hiyo walimtambulisha Bruno GuimarĂ£es kutoka Newcastle, aliyesajiliwa kwa Pauni 75 milioni.
Habari za ndani hata hivyo zinadai kwamba bado Arteta anataka mchezaji wa hadhi ya juu wa nafasi ya winga ya kushoto, matarajio ya awali yalikuwa kwa Vinicius kwa imani kuwa angekuwa na mchango mkubwa.
Arsenal pia inadaiwa kusaka mchezaji mahiri wa nafasi ya ulinzi wakati kukiwa na habari kwamba William Saliba anatarajia kuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu akisumbuliwa na matatizo ya mgongo.
Arteta alikiri timu yake kufanya makosa yaliyosababisha wafungwe mabao matatu jambo ambalo alisema wanatakiwa kulifanya kazi ili kuhakikisha wanakuwa bora kwa kuanzia na wachezaji waliopo.
