New York, Marekani
Ferran Torres ameibuka shujaa baada ya kufunga bao pekee na kuiwezesha Hispania kutoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Argentina na kutwaa Kombe la Dunia 2026.
Iliwachukua Hispania dakika 106 kupata bao hilo licha ya kuutawala mchezo na kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Argentina lakini mashambulizi hayo hayakuweza kuzaa bao kwa dakika 90 za kawaida.
Kikwazo kikubwa kwa Hispania alikuwa kipa wa Argentina, Emilio Martinez ambaye aliokoa michomo kadhaa ya Hispania hadi kumaliza dakika 90 timu hizo zikiwa hazijafungana ndipo zilipoongezwa dakika 30.
Katika dakika 30 za nyongeza Hispania waliendelea kulisakama lango la Argentina huku Argentina wakitumia muda mwingi kujihami kabla hawajaadhibiwa dakika ya 106 na Torres aliyefunga bao kwa shuti kali la mguu wa kushoto.
Bao hilo lilianzia kwa mpira mrefu uliopigwa na Lamine Yamal na kumkuta Nico William ambaye alimuunganishia Torres pasi ya kichwa na Torres kufumua shuti lililomshinda Martinez.
Baada ya kuingia bao hilo, Argentina waliokuwa wamezidiwa kila idara, waliamka na kuanza mashambulizi wakiongozwa na Lionel Messi na kuibua hali ya hofu kwa Hispania.
Messi ambaye alishindwa kuonesha umahiri wake kwa kipindi kirefu, bao la Hispania ni kama lilimpa nguvu ya kuongoza mashambulizi yaliyozaa kona mbili za haraka kwenye lango la Hispania.
Ukiachana na mashambulizi hayo yaliyopamba moto baada ya Argentina kufungwa, kwa dakika zote 120, timu hiyo ilifanikiwa kupiga mashuti mawili tu ya maana langoni mwa Hispania.
Dalili za Hispania kutoka na ushindi zilianza kuonekana mapema kwa namna walivyotawala mchezo na kulisakama lango la Argentina waliokuwa na kazi ya kujihami huku wakishindwa kutengeneza mashambulizi ya maana.
Kasi ya mashambulizi ya Hispania kwenye lango la Argentina ilianza kuonekana mapema dakika za 4 na 5, Lamine Yamal alionesha umahiri lakini mashuti yake mawili yaliishia mikononi mwa kipa Martinez.
Hispania kwa mara nyingine dakika ya 38 ilifanya shambulizi langoni mwa Argentina lakini shuti la chinichini la mguu wa kushoto lililopigwa na Mikel Oyarzabal lilidakwa na kipa Martinez.
Hispania pia mara kadhaa ilifanya mashambulizi yaliyotokea upande wa kushoto kwa beki Cucurella lakini krosi za beki huyo ziliokolewa au kutoka nje ya lango.
MAmbo yalizidi kuwaharibikia Argentina baada ya nyota wao Enzo Fernandes kulimwa kadi ya pili ya njano kwa kucheza rafu na hivyo kutoka uwanjani akiwaacha wenzake 10 kupambana katika dakika 30 za nyongeza.
Hispania ambao mara ya mwisho walilibeba Kombe la Dunia mwaka 2010 katika fainali zilizofanyika nchini Afrika Kusini, pia ndio mabingwa wa Kombe la Ulaya 2024 au Euro 2024.
Fainali za Kombe la Dunia zilianza kutimua vumbi Juni 11, 2026 katika nchi za Canada, Mexico na kuhitimishwa Jumapili, Julai 19, 2026 nchini Marekani kwa mechi iliyopigwa mjini New York kwenye Uwanja wa New Jersey.
Kimataifa Hispania bingwa Kombe la Dunia 2026
Hispania bingwa Kombe la Dunia 2026
Read also
