Madrid, Hispania
Hadithi ya mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland kutakiwa na klabu ya Real Madrid imeibuka tena, safari hii kocha Pep Guardiola na winga Vinicius Jr ‘Vini’ majina yao yakichomoza katika mkakati huo.
Hii si mara ya kwanza Real Madrid kudaiwa kumtaka mshambuliaji huyo lakini safari hii habari hiyo inawahusisha kocha Pep ambaye tayari ameaaga Man City pamoja na winga wa Real Madrid, Vinicius Jr.
Wakati wote jina la Haaland likitajwa kuhusishwa na Real Madrid, Pep alikuwa mtu wa kwanza kupinga taarifa hizo na kusisitiza kuwa Man City haina nia ya kumuuza mshambuliaji huyo.
Pep hakuishia kupinga tu bali pia kukanusha zaidi ya mara moja alichokiita uvumi kuwa Haaland alikuwa akipita tu Man City na kwamba kulikuwa na makubaliano maalum ya mchezaji huyo kwenda Real Madrid baadaye.
Baada ya kuondoka kwa Pep sasa kilichobaki ni kuona nini kitatokea kwa Haaland, atabaki na timu hiyo au ataamua kuondoka kama alivyofanya kocha wake.
Kuhusu Vini upo ukweli kwamba mchezaji huyo hakuwa na furaha msimu uliopita wa 2025-26 hivyo nia ya kuachana na klabu hiyo ni jambo lililo wazi na limekuwa likizungumzwa mara kwa mara.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari, Real Madrid inaamini kuwa mchezaji wa kumsajili baada ya kumuuza Vinicius ni Haaland, mmoja wa washambuliaji wa hadhi ya juu duniani.
Haaland na Vinicius kwa sasa wanaziwakilisha timu zao za taifa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazoendelea Marekani, Mexico na Canada, Vinicius akiiwakilisha Brazil na Haaland, Norway.
Nje ya Pep na Vini, rais wa klabu ya Real Madrid, Florentino Perez aliyechaguliwa kwa mara nyingine hivi karibuni ametangaza mkakati wa kusajili wachezaji wenye majina makubwa ambao anaamini ndio wenye hadhi ya kuichezea timu yake.
Perez hatanii katika hilo, anafahamika vyema hivyo haitoshangaza kuona akikubali kumpiga bei Vini na kumsajili Haaland au akambakisha Vini na Haaland akasajiliwa, kwa Perez hilo ni jambo la kawaida.
Kimataifa Safari ya Haaland Madrid, Pep, Vini watajwa
Safari ya Haaland Madrid, Pep, Vini watajwa
Read also
