Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa timu ya Simba, John Bocco anatarajia kulipwa Sh Milioni 200 baada ya Mahakama Kuu Tanzania kuitaka kampuni ya michezo ya kubahatisha ya Princess Leisure kumlipa mchezaji huyo kiasi hicho cha fedha.
Bocco ambaye pia ni nahodha wa Simba na mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars anatakiwa kulipwa kiasi hicho cha fedha baada ya kampuni hiyo kutumia picha zake katika matangazo yao.
Hukumu hiyo ilitolewa Agosti 31 na Jaji Irvin Mugeta iliitaka kampuni hiyo kulipa kiasi hicho cha fedha licha ya kuwa katika madai ya awali, Bocco alitaka alipwe Sh bilioni 1 kama fidia ya kutumia picha hizo bila ya makubaliano.
Bocco aliyewakilishwa na mawakili Innocent Michael na Gadi Kabele, katika madai yake alidai kwamba kitendo cha kampuni hiyo kutumia picha yake kilimaanisha kwamba alivunja mkataba na klabu ya Simba ambayo ilijiandaa kumchukulia hatua za kinidhamu.
Mchezaji huyo pia alidai kwamba hakuwahi kuipa idhini kampuni hiyo kutumia picha yake na hawakuwa na makubaliano katika jambo hilo.
Jaji Mugeta wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, alihitimisha kwa kuitaka kampuni hiyo kumlipa fidia mchezaji huyo.
Baadhi ya picha zilizotumika na kuonekana katika mtandao wa Instagram ni ile iliyokuwa na tangazo lililowakumbusha mashabiki kuhusu uhondo wa Ligi Kuu NBC.
Tangu kutolewa kwa hukumu hiyo na habari kusambaa kwenye vyanzo mbalimbali vya habari, imesababisha kuibuka kwa mjadala kuhusu hakimiliki na matumizi sahihi ya picha za wanamichezo na wasanii pale picha hizo zinapotumika kibiashara.
Hakimiliki Bocco kulipwa Sh 200 milioni
Bocco kulipwa Sh 200 milioni
Read also
