Paris, Ufaransa
Klabu ya PSG ya Ufaransa inadaiwa kufanya mazungumzo na mshauri wa kocha Jose Mourinho ili kocha huyo akabidhiwe mikoba ya kuinoa timu hiyo kuanzia msimu ujao.
Mourinho ambaye kwa sasa anainoa AS Roma ya Italia, PSG inakuwa timu nyingine ya pili kubwa kuhusishwa naye baada ya timu yake ya zamani ya Chelsea nayo kudaiwa kuwa na mpango huo.
Kocha wa sasa wa PSG, Christophe Galtier licha ya mambo yake kumuendea vizuri kwenye Ligi 1 Ufaransa, matajiri wa klabu hiyo hawafurahii mwenendo wa timu yao hasa baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mipango ya mabosi wa PSG kwa sasa mbali na kumpata kocha mpya mwenye hadhi, pia inajipanga kuwauza baadhi ya wachezaji wakiwamo wenye majina makubwa na kuingiza sura mpya.
Wakati PSG ikimpigia hesabu Mourinho, kocha wa zamani wa timu hiyo, Mauricio Pochettino naye anawindwa na Chelsea ambayo msimu huu umekuwa wa hovyo kwao licha ya kufanya usajili wa bei mbaya.
Chelsea kwa sasa inanolewa na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Frank Lampard ambaye ni kocha wa muda na kilichopo ni kwamba baada ya msimu huu itakuwa na kocha mpya wa kudumu.
Tangu kuanza msimu huu, Chelsea imeshafukuza makocha wawili, wa kwanza ni Thomas Tuchel na wa pili ni Graham Potter na sasa anasubiriwa kocha mpya wa kuanza timu hiyo msimu wa 2023-24.
Kimataifa PSG yamuwania Mourinho
PSG yamuwania Mourinho
Read also
