New York, Marekani
Rais wa Marekani, Donald Trump naye ameibuka na kumlaumu kocha wa England, Thomas Tuchel kwa mbinu alizotumia katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Argentina.
Katika hoja yake hiyo, Trump kwa kiasi kikubwa amehoji majukumu ya ulinzi ambayo Thuchel alimpa mshambuliaji wa timu hiyo, Harry Kane hasa katika kipindi cha pili.
Tuchel ameshutumiwa baada ya England kufungwa mabao 2-1 na Argentina na kutolewa katika hatua ya nusu ya fainali ingawa bado anaungwa mkono na mabosi wa Chama cha Soka England na inaaminika ndiye atakayeiongoza timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Ulaya 2028 au Euro 2028.
England walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Anthony Gordon dakika ya 55 na baada ya hapo Tuchel alijaza mabeki sita nyuma lakini Argentina walimzidi ujanja na kufunga mabao mawili dakika za 85 na 92 (90+2).
Akitoa hoja yake dhidi ya mbinu za Tuchel, Trump awali alianza kwa kumsifia Kane na kukumbushia walivyowahi kucheza naye golfu kwenye ufukwe wa West Palm takriban miezi 18 iliyopita.
“England mna mchezaji mzuri, mchezaji ambaye niliwahi kucheza naye golfu, mnamjua huyo? ni Harry ambaye amekuwa mchezaji mahiri, nafikiri walikosea kumfanya awe mchezaji wa ulinzi,” alisema Trump.
Trump alifafanua akisema kilichotokea ni kwamba England walipata bao la kuongoza na baada ya hapo walichofanya ni kumchukua mchezaji wao bora na kumuweka katika eneo la ulinzi.
