Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Yanga imetozwa faini ya Sh milioni 100 wakati rais wa klabu hiyo, Hersi Said na ofisa mtendaji mkuu wake, Andre Mtine wamepelekwa kamati ya maadili kujieleza.
Adhabu hiyo imetolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) iliyokutana Alhamisi, Julai 2, 2026 na kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi hiyo.
Taarifa ya kamati hiyo iliyopatikana Ijumaa Julai 3, 2026 imeeleza kuwa Yanga imetozwa faini hiyo kwa kosa la kutotumia chumba rasmi cha kubadilishia nguo kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na kutumia nyumba iliyo jirani na uwanja huo.
Yanga katika mechi hiyo ya mwisho ya ligi msimu wa 2025-26 iliyochezwa Jumanne Juni 30, 2026 dhidi ya JKT Tanzania, iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 na kutawazwa rasmi bingwa wa ligi hiyo.
Kuhusu viongozi wa klabu hiyo, wametakiwa kufika kamati ya maadili ili kwenda kujieleza kwa kuwa kosa hilo la uvunjifu wa kanuni limejirudia kwa mara ya pili.
Mwezi Mei mwaka huu, Yanga ilitozwa faini ya Sh 30 milioni 30 kwa kosa hilo hilo la kutotumia vyumba rasmi vya kubadilishia nguo katika mechi yao na Simba iliyochezwa kwenye uwanja huo huo na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Kamati hiyo pia imetoa onyo kali kwa timu ya KMC baada ya wachezaji wake watatu, Aimar Said Twalib jezi namba 71, Steven Donald Mgimwa jezi namba 80 na Hussein Kihiyo jezi namba 86 kwa kuvaa jezi inayozidi namba 70.
Wachezaji hao walivaa jezi hizo katika mechi yao na Simba ambayo walifungwa bao 1-0 na kitendo hicho ni kwenda kinyume na kanuni 17.2 ya ligi kuu inayohusu taratibu za mchezo.
Nayo klabu ya Mtibwa Sugar imetozwa faini ya Sh milioni 5 kwa kosa la wachezaji wake kutotumia chumba rasmi cha kubadilishia nguo kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi katika mechi yao na Namungo FC, mechi ambayo Mtibwa ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-1.
Ligi Daraja la Kwanza
Katika mapitio ya mechi za ligi daraja la kwanza, kamati ilipitia matukio ya mechi kati ya Stand FC Masasi na Pan African na kumfungia mchezaji wa Lindi Soccer Academy, Ramadhan Mlaponi kujihusisha na soka kwa miezi 12.
Mlaponi alifungiwa kwa kosa la kutumia leseni ya Swizan Edwin ambaye ni mchezaji halali wa Stand FC ili apate nafasi ya kucheza mechi hiyo.
Stand FC, timu kutoka Mtwara ambayo ndiyo iliyoshinda mchezo huo kwa bao 1-0, pia imeporwa ushindi huo na Pan African ya Dar es Salaam kupewa pointi tatu na mabao matatu.
Sambamba na hilo, kocha wa Stand FC, Mbano Kizito amefungiwa miezi 12 na kutozwa faini ya Sh 500,000 kwa kumchezesha mchezaji ambaye ni batili kiusajili.
Kimataifa Yanga yatozwa faini Sh milioni 100
Yanga yatozwa faini Sh milioni 100
Read also
