Na mwandishi wetu
Beki wa kati wa Yanga, Ibrahim Bacca amesema mchezo wao wa jana Jumatano dhidi ya Kagera Sugar ulikuwa mgumu kutokana na wapinzani wao kuziba njia zao zote lakini mbinu za kocha wao, Miguel Gamondi ziliwatoa kwenye mtego huo na kuibuka na pointi tatu.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Yanga ililazimika kusubiri mpaka dakika ya 82 kupata bao kupitia kwa Mudathir Yahya na kuendelea kujikita kileleni kwa pointi 68 kwa mechi 26.
“Nadhani ulikuwa mchezo mzuri, na walishtukia Kagera na kuziba njia zote, sehemu zote tunazopitia na wakawa wakakamavu kuanzia mwanzo nadhani mpaka dakika za mwisho lakini kwa ukubwa wetu na maono yake mwalimu alibadili vitu kidogo tukapata ushindi, Muda alitumia vizuri ile nafasi tuliyoipata,” alisema Bacca.
Beki huyo pia alisema kuwa licha ya kuuona kidogo mwanga wa ubingwa kwa mara nyingine msimu huu lakini anaamini bado wanahitaji kuongeza nguvu na umakini katika mechi zao zilizosalia ambazo nyingi watacheza ugenini dhidi ya timu zinazopigania vitu tofauti katika ligi hiyo.
Yanga imebakisha michezo minne kufunga rasmi pazia la ligi kwa kuumana na Mtibwa Sugar Mei 13 na Dodoma Jiji Mei 22, mechi zote mbili zikiwa ugenini kabla ya kurejea nyumbani kuvaana na Tabora United Mei 25 na Tanzania Prisons Mei 28, mwaka huu.
Soka Bacca akiri Kagera wagumu
Bacca akiri Kagera wagumu
Read also
