Na Hassan Kingu
Ushindi wa timu ya wanawake ya Hispania kwenye Kombe la Dunia umeibua mjadala wa nje ya soka baada ya mshambuliaji wa timu hiyo, Jenni Hermoso kupigwa busu mdomoni na aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Hispania, Luis Rubiales.
Dunia ya soka ilipumzishwa kufurahia na kujadili ubingwa wa timu ya wanawake ya Hispania, ubingwa uliopatikana Agosti 20, badala yake mjadala mkali uliozua taharuki ukawa ni kuhusu Luis kumpiga busu Jenni.
Ni kama ilivyokuwa mwaka 2006, timu ya wanaume ya Italia ilipobeba Kombe la Dunia, mjadala wa ushindi ulipoozeshwa na tukio la beki wa Italia, Marco Materrazi kupigwa kichwa na kiungo wa Ufaransa, Zinedine Zidane.
Tofauti ya mijadala hiyo ni kwamba Zidane au Zizou alijutia alichokifanya lakini Luis hakujutia, licha ya kusakamwa na kutakiwa ajiuzulu badala yake alisema kwamba furaha iliyopitiliza ndiyo iliyomfanya ampige Jenni busu la mdomoni.
Busu hilo likazua taharuki na kuibua shinikizo kila kona la kumtaka Luis ajiuzulu kwa kumpiga busu mwanamke ambaye huenda wapo wanaume wengine wengi waliotamani kufanya hivyo lakini hawajawahi kuipata nafasi ambayo Luis aliipata na Luis mwenyewe amegoma kujiuzulu huku hoja yake ikisimamia katika makubaliano baina yake na Jenni kwamba hakumpiga busu Jenni kwa lazima, walikubaliana.
Mjadala ukashika kasi, mashinikizo ya kumtaka Luis ajiuzulu yakaongezeka siku hadi siku, kuanzia kwa Waziri Mkuu wa Hispania, mawaziri, wanasoka wanawake na makundi mbalimbali ya wanaharakati.
Yote hayo hayakumshtua Luis, aliendelea kushikilia msimamo wa kutokuwa tayari kujiuzulu kabla ya Fifa kuingilia kati na kumsimamisha kujihusisha na masuala ya soka kwa siku 90.

Ikafuatua ofisi ya mwendesha mashtaka kutangaza kusudio la kumshitaki wakati huo huo, Jenni naye alishatangaza nia yake ya kufanya hivyo kwa alichokidai kwamba hakupenda alichofanyiwa na Luis.
Baada ya mashinikizo kuongezeka nje ya Hispania wakiwamo wachezaji wanawake kugoma kuichezea timu ya taifa kama Luis angeendelea kuwa madarakani, hatimaye Luis akakubali yaishe, akatangaza kujiuzulu.
Kujiuzulu kwa Luis hakujazuia mjadala kuendelea, bado watu wanahoji je ni kweli Luis alifanya kosa au tatizo limekuzwa bila sababu?
Watetezi wa Luis
Wanaomtetea Luis wanadai kwamba alichokifanya kilikuwa na ridhaa ya Jenni na wanatumia moja ya picha za tukio hilo kutetea hoja yao, picha inayotajwa ni ile inayoonesha mkono wa kulia wa Jenni ukimshika Luis kiunoni.
Katika picha hiyo kinachoonekana kimetafsiriwa kuwa ni Jenni kumpa ushirikiano Luis, kwa maana nyingine hakuwa na tatizo kwa alichofanyiwa na Luis.

Watetezi hao pia wanaona kama Jenni ameangukia katika shinikizo la watu ambao hawakupenda kile kilichofanywa na Luis na kwamba awali hakuliona jambo hilo kuwa ni lenye ubaya.
Hapa inajengwa hoja kwamba Luis alifurahia baada ya Hispania kubeba kombe la dunia, akafurahishwa na soka la Jenni, akaona kumkumbatia haitoshi bali busu lingeonesha alivyokuwa na furaha, na Jenni picha zinamuonesha akimpa Luis ushirikiano.
Zaidi ya yote hayo hakuna picha ya Jenni iliyomuonesha akiwa amekunja uso baada ya kupigwa busu la mdomoni hivyo hakuwa na tatizo na jambo hilo.
Mama wa Luis amekuwa mstari wa mbele kumtetea mwanaye ikiwamo kufanya mgomo wa kula na hoja yake ni moja tu kwamba mwanaye hakuwa na kosa kwani tukio zima lilifanyika kwa makubaliano baina ya Luis na Jenni.
Wanaompinga Luis
Wanaompinga Luis wanakataa kuwapo makubaliano baina yake na Jenni badala yake wanaliona tukio zima kama ni unyanyasaji na udhalilishaji mwanamke lililofanywa na kiongozi wa soka na suluhisho lake ni kumuondoa kiongozi huyo madarakani.
Hoja nyingine ya kundi hili pia inahusisha picha ile inayomuonesha Jenni akiwa ameiondoa mikono yake kwenye kiuno cha Luis, ni kama vile kwanza kukubali kukumbatiwa lakini hapo hapo kulikataa busu la mdomoni.
Kundi hili linamuweka Luis katika kundi la wanaume wanaodhalilisha wanawake na kuwakosea heshima kwa kutumia nafasi zao, ni kundi ambalo pia limekuwa likishinikiza mabadiliko ya kiungozi katika idara mbalimbali za Shirikisho la Soka Hispania.

Luis pamoja na kukubali kujiuzulu uongozi katika Shirikisho la Soka Hispania, bado ana kesi ya kujibu baada ya kushitakiwa na vyombo vya kisheria nchini Hispania.
Tumejifunza nini?
Tukio zima hili linatufundisha kuwa kuna mambo ambayo mtu hufanyiwa kwa ridhaa yake, tofauti na hivyo ni kesi kubwa. Tumefundishwa kuheshimu mipaka kati ya mwanamke na mwanaume.
Awali wengi wetu hatukutarajia kuona dunia ya soka ikijadili busu ambalo kiongozi wa soka ameamua kumpiga mchezaji wake tena baada ya kuvutiwa na soka la mchezaji huyo kwenye timu ambayo imebeba taji la dunia.
