Madrid, Hispania
Hatma ya kocha wa wanawake wa timu ya Hispania, Jorge Vilda (pichani juu) huenda akatimuliwa baada ya kuwapo habari kwamba Shirikisho la Soka Hispania (REEF) linaangalia uwezekano wa kuchukua uamuzi huo.
Vilda aliyeiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Dunia, ni mtu pekee kwenye benchi la ufundi la timu hiyo aliyebaki katika nafasi yake baada ya wasaidizi wake wote kujiuzulu wakishinikiza kujiuzulu kwa Rais wa REEF, Luis Rubiales aliyembusu mshambuliaji wa timu hiyo, Jenni Hermoso.
Wachezaji 81 wa Hispania wakiwamo 23 walioiwezesha timu hiyo kubeba Kombe la Dunia wameahidi kutoichezea timu hiyo tena kama Rubiales ataendelea kuwa kwenye nafasi ya urais wa shirikisho hilo ingawa tayari Fifa imemsimamisha Rubiales kwa siku 90.
Vilda alionekana kwenye mkutano mkuu maalum wa REEF akimpongeza Rubiales kwa msimamo wake wa kutojiuzulu lakini baadaye alibadili msimamo na kuanza kukosoa alichokifanya Rubiales.
Mabosi ndani ya REEF wanaamini kwamba mwenendo mzima wa tukio hilo unatosha kuwa sababu ya kumtimua Vilda katika nafasi yake.

Jumatatu iliyopita, viongozi REEF walifanya mkutano mkuu maalum ulioongozwa na kaimu rais wa shirikisho hilo, Pedro Rocha na kujadili mpango wa kulifanyia maboresho shirikisho hilo kwa lengo la kuwa na mwanzo mpya.
Habari za ndani zinadai kwamba baadhi ya wajumbe wa mkutano huo hawataki kumshinikiza Rubiales ajiuzulu kwa lazima badala yake walitoa taarifa kama ya kumshauri achukua uamuzi huo jambo ambalo hadi sasa Rubiales hajakubaliana nalo.
Rubiales, 46, amejikuta akishutumiwa kila kona kwa kitendo chake cha kumbusu mdomoni Jenni baada ya Hispania kuichapa England bao 1-0 na kubeba Kombe la Dunia.
Baadaye Rubiales alisema kwamba alimpiga busu mchezaji huyo baada ya kuwa na furaha isiyo kifani na kutaka wenye tafsiri tofauti wapuuzwe lakini amejikuta akisakamwa sehemu mbalimbali duniani na alichofanya kutafsiriwa kuwa ni udhalilishaji wa kijinsia.
