Geneva, Uswisi
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limemsimamisha kwa siku 90, Rais wa Shirikisho la Soka Hispania (REEF), Luis Rubiales wakati kamati yake ya nidhamu ikimchunguza kwa kosa la kumbusu mdomoni mshambuliaji wa timu ya Taifa, Jenni Hermoso.
Siku chache zilizopita Fifa ilitangaza kufanya uchunguzi wa kadhia ya Rubiales kumbusu mchezaji huyo mdomoni Jumapili iliyopita wakati wachezaji wa Hispania wakikabidhiwa medali baada ya kuibwaga England bao 1-0 na kubeba Kombe la Dunia la Wanawake (WWC).
Uamuzi wa Fifa umekuja baada ya Rubiales kukataa kujiuzulu licha ya kuwapo malalamiko kumtaka afanya hivyo kutoka kwa watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa Serikali ya Hispania na wanasoka wanawake wa klabu mbalimbali ndani na nje ya Hispania.
Kitendo cha Rubiales (pichani juu) kumbusu mchezaji huyo mdomoni wakati wa shamrashamra za ushindi ikiwamo kumshika shingoni licha ya kuibua mjadala lakini mwenyewe alijitetea akidai kilitokana na furaha iliyopitiliza.
Awali Jenni alionekana kumtetea Rubiales lakini baadaye akadai hakulipenda jambo hilo na kwamba halikufanyika kwa ridhaa yake na tayari wanasoka wanawake wameitisha mgomo wa kutoichezea timu ya Hispania kama kiongozi huyo ataendelea kuwa madarakani.
Taaifa ya Fifa iliyopatikana Jumamosi hii ilieleza kwa kifupi kuwa Rubiales ameondolewa madarakani kwa siku 90 ili kupisha uchunguzi ulioanza kufanywa Alhamisi iliyopita.
Fifa pia iliwataka viongozi wa REEF pamoja na Rubiales katika siku hizo 90nkutofanya mawasiliano yoyote na Jenni,

Baada ya uamuzi wa Fifa, REEF imempitisha makamu rais wake, Pedro Rocha kukaimu nafasi hiyo na kufafanua kwamba Rubiales ana imani na uchunguzi wa Fifa ambao pia utampa nafasi ya kujitetea kwa kosa analodaiwa kulifanya.
Adhabu hiyo pia unamuondoa kwa muda Rubiales katika nafasi yake ya makamu rais wa Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) na hatotakiwa kujihusisha na masuala ya soka kwa kipindi chote cha siku 90.
Rubiales mwenye umri wa miaka 46, iwapo atakutwa na hatia katika kadhia hiyo, anaweza kukutana na adhabu ya kuondolewa kabisa madarakani, kuonywa au kutozwa faini, kimoja kati ya hivyo au vyote kwa pamoja.
Wakati huo huo makocha wasaidizi na maofisa wa benchi la ufundi la timu ya wanawake ya Hispania iliyobeba Kombe la Dunia wote wamejiuzulu nafasi zao isipokuwa kocha mkuu Jorge Vilda, makocha hao wote wanapinga Rubiales kuongoza REEF,
Waliojiuzulu ni makocha wasaidizi, Montse Tome, Javier Lerga na Eugenio Gonzalo Martin, mwingine ni kocha wa viungo Blanca Romero Moraleda na kocha wa makipa Carlos Sanchez. Pia wamo makocha wengine sita waliokuwa na timu hiyo katika ngazi mbalimbali kuanzia timu za vijana, nao wamejiuzulu.
