*Amkumbuka Matumla
Jina la Dula Mbabe ni maarufu katika ngumi hasa anapohusishwa na mpinzani wake Twaha Kiduku, awali baadhi ya mashabiki walianza kuuhusisha upinzani wao kama ule wa Rashid Matumla au Snake Boy na Maneno Oswald au Mtambo wa Gongo.
Ni kwa bahati mbaya mjadala wa Dula Mbabe kwa sasa umekuwa ukihusisha zaidi vipigo anavyovipata na hivyo kuanza taratibu kufuta matarajio ya kuwapo upinzani mkali kati yake na Kiduku kama ule wa Snake Boy na Mtambo wa Gongo.

Na ingawa majigambo ya Dula Mbabe kabla ya pambano yamekuwa yakiwapa mashabiki wake matumaini makubwa ya ushindi lakini hali imekuwa tofauti kwani amekuwa akishindwa kutamba.
Kashindwa kutamba kwa Kiduku, ikajengeka dhana kwamba Kiduku alibebwa lakini kushindwa katika pambano lake la mwisho dhidi ya bondiaTshimanga Kantompa kutoka DR Congo, kumeibua mapya, wako wanaomtaka aachane na jina la Mbabe, aitwe tu kwa jina lake la Abdallah Pazi lakini wapo wanaomtaka astaafu ngumi, hoja ambayo imemuibia Mtambo wa Gongo.
“Hapana, si sahihi Dula Mbabe bado mdogo kwenye ngumi wazo la kustaafu ngumi si zuri badala yake ni vyema akae na kujiuliza kulikoni anapigwa vipigo mfululizo,’’ anasema Maneno katika mazungumzo yake hivi karibuni na Green Sports.
“Wanaotaka Mbabe astaafu ngumi watambue kwamba ngumi ni kazi na kama Mbabe ameichagua ngumi kuwa kazi yake kumtaka astaafu mapema ni kumnyima fursa ya kupata kipato,’’ anafafanua.
Maneno anasema kwamba anachotakiwa kufanya Mbabe nikubadili staili ya upiganaji, inawezekana wapinzani wake wameshamsoma, wanajua udhaifu wake hivyo wanautumia kumpiga.
Akifafanua zaidi Maneno anasema kuna wakati kipigo hakiepukiki kwa kila bondia lakini unapopigwa mfululizo hata mashabiki wako unawakatisha tamaa hivyo ni muhimu kujiuliza kulikoni.
Akitolea mfano pambano la Mbabe na bondia kutoka DR Congo, Maneno anasema, Mbabe alianza kupigwa kuanzia raundi ya kwanza na hakuona ngumi yoyote ya maana kutoka kwa bondia huyo na hata sare aliyotoka na Kiduku ameonyesha udhaifu, aitumie ile na mapambano mengine aliyopigwa katika maandalizi yake.
Maneno pia alieleza kushangazwa kwake na aina ya ngumi zinazomuangusha Mbabe, “ngumi inayotokea pembeni mara nyingi haina nguvu sana kama ile ya moja kwa moja, sasa Mbabe amekuwa akiangushwa kwa ngumi zinazotokea pembeni si zile za mbele moja kwa moja, hili nalo ni jambo analotakiwa kulifanyia kazi na kujiuliza tatizo ni nini hasa.”
“Mbabe pia naona kama anatumia nguvu nyingi, hawasomi wapinzani wake, ni vizuri kumsoma mpinzani badala ya kutumia nguvu nyingi, kuna mpinzani unapotumia nguvu nyingi unakuwa umemrahisishia kazi kwani atakuwa anakuzungusha tu ulingoni na kuzidi kukuchosha kabla ya kukupiga ngumi za pointi.

Katika hilo Maneno anamtaja Matumla akidai kuwa kuna wakati alikuwa kama anamzungusha mpinzani ulingoni na hapo ukiwa mwenye kutumia nguvu utachoka na mwisho kushindwa pambano.
Maneno pia alimtaka Mbabe kupunguza mapambano ya mara kwa mara, “kweli kuna kuhitaji pesa lakini mapumziko nayo yana umuhimu wake katika kujiandaa na pambano jingine, na hapa bila shaka pambano lake na bondia wa DR Congo limethibitisha hilo.
Kuhusu majigambo ya Mbabe, Maneno anasema hilo haliepukiki kwani bondia hawezi kuingia ulingoni kinyonge, amekubali kupigana maana yake ni kwamba anajiamini hivyo ni lazima ajigambe atakapoulizwa, na si sahihi kuwa mnyonge kabla ya pambano au kuonyesha kwamba utapigwa.
Hata hivyo, Maneno anatahadharisha kwamba hiyo haina maana ya kulewa sifa, “sina maana kwamba bondia huyo alewe sifa na kujiamini kupita kiasi kwamba lazima atashinda pambano, hapana ni lazima kuchukua tahadhari, kujiandaa vizuri na kutomdharau mpinzani wako lakini inapotokea ukaulizwa kabla ya pambano ni lazima useme kwa kujiamini na kwamba utashinda.
Upinzani na Matumla
Akizungumzia upinzani wake na Matumla, Maneno anasema kwamba wakati ule ilikuwa kama Simba na Yanga kwenye soka, yeye akitajwa kuwa Yanga na Matumla Simba
Anasema kwamba hali ile haikuwa ulingoni tu bali hata mitaani kwao kwenye vitongoji vya Keko jijini Dar es Salaam, “iwe Keko Machungwa, Keko Akida na kwingineko hadithi kubwa jioni baada ya pambano ilituhusu mimi na Rashidi (Matumla),’’ anasema.
Akimzungumzia Matumla, Maneno anasema alikuwa bondia bora na mpinzani wake waliyechoshana, hapohapo anayakumbuka mapambano yao mawili yaliyopigwa miaka ya 2000 mwanzoni kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere zamani PTA.
Katika mapambano hayo, Maneno alimpiga Matumla katika pambano moja akapigwa katika pambano la pili. “Unajua unapocheza na bondia bora kila mtu anaamini utapigwa sasa mimi nilipompiga Matumla ikawa habari kubwa, kama unavyojua haikuishia ulingoni tu bali hata katika mitaa ya Keko mashabiki wangu walikuwa wakijivunia.
Akizungumzia siku aliyopigwa, Maneno anakiri kwamba ushindi wa pambano lao la kwanza ulimfanya alewe sifa na kujiona ana uwezo wa kumpiga Matumla hasa kwa kuwa watu walimsifia sana, “nilikuwa nasifiwa kila siku, na hiyo ni kwa sababu nilimpiga bondia bora.
Zaidi ya hilo, Maneno anasema kwamba alicheza akiwa anaumwa mkono na licha ya daktari wake kuhangaika na kumpatia tiba iliyomsaidia kujiona yuko vizuri lakini akiwa ulingoni baada ya kurushiana ngumi na mpinzani wake, mkono ulianza kuuma tena. “kama unavyojua nilikuwa na ngumi nzito lakini siku ile nacheza na Rashid (Matumla) hali ilikuwa tofauti, mkono ulinisumbua ingawa nilichomwa sindano lakini baadaye hali haikuwa nzurilakini pia nililewa sifa.
Tofauti na hali hiyo, Maneno anasema mapambano yake na Matumla yanabaki kwenye kumbukumbu zake kwa kuwa ndio mapambano pekee ambayo walau anaweza kusema yalimpa kipato cha kumfurahisha tofauti na mengine.
“Nimecheza ngumi muda mrefu tangu miaka ya 1990 lakini ni mapambano yangu na Matumla tu ambayo nilipata kati ya shilingi milioni mbili hadi tatu, hiyo ni baada ya kutoa pesa za wasaidizi wangu katika mazoezi na gharama nyingine za maandalizi,’’ anasema.
Maneno pia anasema kwamba nje ya pesa hizo ambazo hutolewa na pomota kuna pesa nyingine kutoka kwa mashabiki ambazo hazihusiani na zile za promota.
Akifafanua anasema baada ya kumpiga Matumla kuna mashabiki walikuwa wakimuita kwenye maofisi yao na kumpa pesa, “unaitwa halafu unakabidhiwa bahasha ndani ina shilingi 200,000 au 300,000, na kupongezwa kwa ushindi dhidi ya Matumla.”
Nje ya mapambano yake na Matumla, Maneno anasema katika mapambano mengine hakuwahi kupata zaidi ya shilingi 500,000 na mara nyingi ilikuwa ni chini ya 500,000.
Akizungumzia ngumi enzi zao, Maneno anasema mabondia waliibiwa sana na mapromota lakini pia ngumi za kulipwa zilitawaliwa na migogoro ya mara kwa mara, kila mtu alijiona ana haki ya kusimamia ngumi.
Anasema jambo hilo kwa kiasi fulani lilichangia mabondia kudhulumiwa kwani hakukuwa na sauti moja ya kuwasimamia, “unaenda nje ya nchi kupigana unaambiwa thamani ya pambano lako ni dola 20,000 kwa mfano lakini hadi unarudi Tanzania mfukoni una dola 1,000 tu au hata pungufu ya hiyo.”
“Wakati mwingine unaenda hata mkataba wako hujauona, unaishia kwenye ufahari wa kupanda ndege na kulala hoteli ya hadhi ya juu nje ya nchi, kwa kweli kipindi kile tulidhulumiwa sana, ukitaka kujua hilo muangalie Matumla, kapeperusha bendera ya Taifa nje, kapewa heshima hadi kwenda Ikulu lakini hali yake kwa sasa haitoi dalili zozote za bondia bora wa zamani.
Pamoja na madhila yote hayo waliyofanyiwa, Maneno anashukuru kwani yote yaliyowapata yamekuwa kama somo lenye maana kwani kwa sasa hali ni tofauti, sisi ni kama tulizitoa ngumi gizani kwani kwa sasa kuna kila ishara ya kuwapo mwanga.
Maneno anashauri mabondia wa zamani wakumbukwe na kuthaminiwa na Serikali kwa hilo lakini pia washirikishwe katika mambo mbalimbali yanayohusu ngumi nchini.
Kuhusu anachojivunia kwenye ngumi Maneno anasema bila kupepesa macho, “Bila kukuficha sina la kujivunia zaidi ya kujulikana, kweli nimejenga kibanda changu Kongowe lakini ukiniuliza la kujivunia nitakwambia ni kujulikana tu, ukipita mitaani utasikia Mtambo wa Gongo huyo au ukiwa na jambo lako utapata urahisi, ni hilo tu.
Nini ushauri wake kwa mabondia wanaochipukia? Hapo Maneno anawapa tahadhari, “wasijiingize kwenye ngumi kwa ajili ya kushiriki kwenye matukio ya kihalifu, tunawajua wengi sipendi kuwataja kwa majina ambao ngumi wamezitumia kushiriki uhalifu ikiwamo ujambazi na ubabe mitaani lakini wameuliwa hivi hivi, kwa hiyo na hawa mabondia watambue kwamba ngumi ni kama ilivyo soka, ni ajira kuna ambao wameneemeka kwa kupata ajira kupitia kwenye ngumi, wako askari polisi, magereza na wengineo.’’
