Na mwandishi wetu
Yanga hatimaye imetwaa taji la Ligi Kuu NBC msimu wa 2025-26 na kuweka rekodi ya kulitwaa taji hilo mara ya tano mfululizo.
Mafanikio hayo yamekuja baada ya kuilaza JKT Tanzania mabao 3-0 katika mechi ya mwisho ya ligi hiyo iliyochezwa Jumanne, Juni 30, 2026 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamhuyo, Dar es Salaam.
Baada ya ushindi huo, Yanga imekamilisha mechi za ligi hiyo ikiwa na pointi 75 wakati mahasimu wao Simba waliokuwa wakitoa ushindani wameishia kumaliza ligi nafasi ya pili na pointi 73 baada ya kuichapa KMC bao 1-0.
JKT waliuanza mchezo kwa kujiamini na kuonesha dalili zote za kuizuia Yanga kuweka rekodi ya kulibeba taji hilo lakini mambo yakaanza kuwa tofauti katika dakika ya nane kwa Yanga kupata bao ambalo lilifungwa na Prince Dube baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Max Nzengeli.
Wakati Yanga ikisaka bao la kuongeza na JKT ikisaka bao la kusawazisha, Yanga walipata pigo dakika ya 45 baada ya kiungo wao Pacome Zouzoua kuumia alipochezewa vibaya na beki wa JKT, Hassan Wahabi.
Tukio hilo lilisababisha kuwapo hali ya huzuni kwa wachezaji wa timu zote ambao walionekana kumsikitia Pacome wakati akipewa huduma ya kwanza kwa kilichoonekana kuwa alipata maumivu makubwa.
Mwamuzi wa mchezo huo Hassan Katanga awali alimpa kadi ya njano beki huyo wa JKT lakini baadaye aliifuta na kumpa nyekundu.
Dakika tano baada ya timu kutoka mapumziko, Yanga walipata bao la pili lililofungwa na Max Nzengeli, bao lililotokana na krosi ya chini iliyopigwa na Allan Okello.
Yanga walikamilisha bao la tatu lililofungwa na Depu katika dakika ya 60 na baada ya kufunga bao hilo aliinua juu jezi ya Pacome akiwaonesha mashabiki wa Yanga.
KMC yapewa kipigo cha mwisho
Wakati Yanga wakipata ushindi wa mwisho uliowapa taji hilo, KMC wao walipewa kipigo cha mwisho cha kuaga ligi hiyo walipofungwa bao 1-0 na Simba.
Bao hilo pekee la ushindi kwa Simba lilipatikana katika dakika ya 55 kwa mkwaju wa penalti, mfungaji akiwa ni Jospin Loemba.
KMC sasa inaaga rasmi ligi hiyo pamoja na Mtibwa Sugar wakati mechi za play off za kuwania kubaki katika ligi hiyo zitawahusisha mafahari wa jiji la Mbeya timu za Prisons na Mbeya City zilizomaliza nafasi ya 13 na 14.
Matokeo ya mechi za mwisho za ligi hiyo ni kama ifuatavyo…
Azam 2-0 Dodoma Jiji
Mashujaa 0-1 Prisons
Namungo 2-1 Mtibwa
Mbeya City 0-0 TRA United
Coastal Union 2-1 Pamba Jiji
Fountain Gate 4-3 Singida BS
Kimataifa Yanga yabeba taji la tano ligi kuu
Yanga yabeba taji la tano ligi kuu
Read also
