Na mwandishi wetu
Kila timu ikiwa imebakiza mechi moja kabla ya kufungwa pazia la Ligi Kuu NBC msimu wa 2025-26, mafahari wa soka Tanzania, Simba na Yanga wameendelea kuwashiana moto kila timu ikinyakua pointi tatu za lala salama.
Timu hizo zimeingia dimbani Jumamosi Juni 27, 2026, Yanga ikiwa Uwanja wa KMC, imeendelea kuimarisha nia yake ya kulibeba taji hilo kwa mara ya tano mfululizo kwa kuilaza TRA United mabao 3-0.
Simba nao wakiwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, hawajakata tamaa, wameendelea kuikomalia Yanga kwa kukoleza ushindani wa taji hilo baada ya kuichapa Singida Black Stars mabao 2-0.
Matokeo hayo maana yake ni kwamba timu hizo zinaendelea kupambana katika nafasi ya kwanza na ya pili zikipishana kwa tofauti ya pointi mbili tu.
Yanga imekomaa kwenye usukani wa ligi hiyo yenye timu 16 ikiwa na pointi zake 72 wakati Simba inayoshika nafasi ya pili ina pointi 70, timu zote hizo kila moja imeingia dimbani mara 29.
Simba walianza kuzitikisa nyavu za Singida BS kunako dakika ya 28 kwa bao lililofungwa na Elly Mpanzu na kuifanya timu hiyo iende mapumziko ikiwa mbele kwa bao hilo pekee.
Kipindi cha pili timu zote zilionesha uhai, Simba wakisaka bao la kuongeza na Singida wakihaha kusawazisha lakini walikuwa ni Simba walioongeza bao la pili na la ushindi lililofungwa na Anicet Oura katika dakika ya 59.
Okelo apiga hat trick ya kwanza ligi kuu
Nyota ya mshambuliaji wa Yanga, Allan Okello kutoka Uganda imeendelea kung’ara baada ya kufunga mabao matatu peke yake (hat trick) katika ushindi wa timu hiyo dhidi ya TRA.

TRA, moja ya timu iliyokuwa ikitajwa kuipa ushindani Yanga haikuweza kuwa tishio badala yake ikakutana na kipigo kama walichopewa Azam FC, timu nyingine iliyokuwa ikitajwa kutishia nafasi ya Yanga kubeba taji mara ya tano mfululizo.
Okello ambaye pia alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo, alifunga mabao hayo peke yake dakika za 28, 51 na 57 na kuipa Yanga ushindi ambao mashabiki wa timu hiyo wanaamini baada ya Azam na TRA hakuna timu nyingine yenye uwezo wa kuwazuia kubeba taji la tano mfululizo.
Matokeo ya mechi nyingine za ligi hiyo ni kama ifuatavyo…
Pamba Jiji 1-2 JKT Tanzania
Coastal Union 0-2 Azam FC
Dodoma Jiji 1-1 Mbeya City FC
Namungo 0-0 Fountain Gate FC
Mashujaa FC 2-0 KMC FC
Prisons 2-1 Mtibwa Sugar
