Miami, Marekani
Vinicius Jr amefunga mabao mawili kati ya matatu na kuipa Brazil ushindi wa 3-0 dhidi ya Scotland lakini kivutio kingine katika ushindi huo ni kuonekana uwanjani kwa mshambuliaji Neymar Jr akiiwakilisha Brazil.
Ushindi huo umeiwezesha Brazil kufuzu moja kwa moja hatua ya mtoano ya fainali za Kombe la Dunia 2026 huku Neymar akikiwakilisha kikosi hicho kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu.
Zikiwa zimebakia dakika 21 kumalizika mchezo huo uliochezwa Alhamisi Juni 25, 2026, kocha wa Brazil, Carlo Ancelotti aliamua kumpa nafasi Neymar ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo.
Mashabiki wa Brazil walimpokea kwa shangwe mshambuliaji huyo aliyeonekana uwanjani na jezi ya timu hiyo mara ya mwisho mwaka 2023 huku akionekana mwenye shauku iliyopitiliza.
Akizungumzia hali ilivyokuwa Neymar anayeongoza kwa kuifungia timu ya taifa Brazil mabao mengi, alisema wakati akiinuka kwenye benchi kujiandaa kuingia uwanjani, moyo wake ulijaa shauku kubwa.
“Moyo ulikuwa ukinienda mbio kwa shauku, lakini nina furaha na kujivunia kwa kuwa kila kitu kilikwenda vizuri,” alisema Neymar.
Kwa Neymar hizi ni fainali zake za nne za Kombe la Dunia lakini alikosa mechi mbili za awali kutokana na matatizo ya misuli ya nyuma ya paja la mguu wa kulia ambayo imekuwa ikimsumbua lakini alipoulizwa kama alikuwa fiti, alijibu,”fiti asilimia 100. asilimia 100”
Katika ushindi wa Brazil, mbali na Vinicius aliyefunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza, bao jingine la timu hiyo lilipatikana dakika ya 60 mfungaji akiwa ni Matheus Cunha.
Kwa Vinicius mabao hayo yanamfanya awe mchezaji wa tano kuifungia Brazil katika mechi za hatua ya makundi za fainali za Kombe la Dunia akiwa ametanguliwa na wakongwe, Jairzinho mwaka 1970, Romario (1994) na Ronaldo na Rivaldo waliofanya hivyo mwaka 2002.
Katika vipindi vyote hivyo vya nyuma, Brazil ilifanikiwa kubeba Kombe la Dunia na swali lililopo ni je safari hii Brazil itaweza tena kubeba taji hilo?
