Guadalupe, Mexico
Kocha mpya wa timu ya taifa ya Tunisia, Herve Renard ameanza vibaya majukumu yake na timu hiyo baada ya kufungwa mabao 4-0 na Japan na kuziaga rasmi fainali za Kombe la Dunia 2026.
Renard, kocha wa zamani wa timu za taifa za Zambia, Ivory Coast na Saudi rabia alipewa jukumu hilo baada ya mtangulizi wake Sabri Lamouchi kutimuliwa kufuatia kipigo cha mabao 5-1 dhidi ya Sweden katika mechi ya kwanza ya timu hiyo.
Tunisia iliumana na Japan katika mechi ya hatua ya makundi iliyopigwa Jumapili Juni 21, 2026 ikiwa na matumaini ya kusahihisha makosa ya mechi ya kwanza lakini mambo hayakuwa mazuri.
Japan waliutawala vyema mchezo na kuandika bao la kwanza dakika ya nne kwa bao la shambulizi la kushtukiza lililofungwa na nyota wa Crystal Palace, Daichi Kamada.
Dakika ya 31, Japan waliongeza bao la pili mfungaji akiwa ni Ayase Ueda ambaye alifumua shuti lililopita miguuni mwa beki mmoja wa Tunisia kabla ya kujaa wavuni.
Mambo yalizidi kuiharibikia Tunisia na kujikuta ikifungwa bao la tatu na Junya Ito dakika ya 69, bao alilofunga kwa kumchambua kipa wa Tunisia, Aymen Dahmen akiwa naye ana kwa ana wakati bao la nne la Japan lilifungwa kwa mara nyingine na Ueda katika dakika ya 83.
Kwa ushindi huo Japan wamefikisha pointi nne na wana nafasi kubwa kusonga mbele hatua ya mtoano ingawa bado wana kazi ya kufanya katika mechi yao ya mwisho ya makundi dhidi ya Sweden hapo Ijumaa wakati Tunisia ambao wameziaga fainali hizo watakamilisha ratiba kwa kuumana na vinara wa kundi lao, Uholanzi.
Baada ya mechi ya kukamilisha ratiba Tunisia wataanza kujiuliza kuhusu mambo ya baadaye ya timu yao hasa kama wanahitaji kuendelea na kocha Herve au kutafuta kocha mwingine.
Kimataifa Kocha mpya Tunisia aanza vibaya
Kocha mpya Tunisia aanza vibaya
Read also
