Vancouver, Canada
Wakati wakijiandaa kuikabili New Zealand, kocha wa timu ya taifa ya Misri, Hossam Hassan (pichani) anajivunia timu hiyo akisema anaamini wameanza kuvuna matunda ya mpango wa maendeleo wa muda mrefu.
Misri au Pharaohs itaumana na New Zeland katika mechi ya Kundi G ya fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazoendelea katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.
Akizungumza kabla ya mechi hiyo itakayochezwa Jumatatu Juni 22, 2026, Hassan alisema wamekuwa wakiijenga timu hiyo hatua kwa hatua kupitia mashindano mbalimbali.
Hassan ambaye alikuwa mshambuliaji wa timu hiyo na klabu kadhaa nchini Misri, alisema kazi ya kuijenga timu hiyo ilianza mapema kabla ya fainali za Kombe la Dunia 2026.
“Tulianza zamani kabla ya Kombe la Dunia, tulipitia kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia, mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Morocco na mechi za kirafiki dhidi ya Saudi Arabia, Hispania na Brazil,” alisema Hassan.
Alisema malengo yake tangu akabidhiwe timu hiyo yamekuwa ni kujenga kikosi ambacho kitaweza kucheza soka lenye hadhi ya nchi hiyo yenye utajiri wa mila zake.
Hassan alifafanua kwamba hata kabla hajawa kocha wa Misri alichotaka ni kuona timu hiyo inacheza soka katika ubora na kwamba mafanikio ya aina hiyo yanahitaji muda.
“Maendeleo haya yanahitaji muda, inamaanisha kuingiza vizazi vipya na kuviongeza kwenye timu jambo ambalo si rahisi hasa pale chaguo lako kubwa linapotoka kwa wachezaji wa ligi ya ndani,” alisema Hassan.
Alibainisha kuwa hafanyi kazi kwa mafanikio ya muda mfupi badala yake anaangalia mambo ya kesho akitaka Misri icheze soka linalofanana na hadhi ya soka la Misri ili kukidhi matakwa ya watu wa Misri.
Misri walizianza fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa sare dhidi ya Ubelgiji, matokeo ambayo si mabaya na mwendelezo wa mafanikio zaidi kwenye mechi na New Zealand ndio wanaoutaka ili kuweka hai matumaini yao ya kufuzu hatua ya mtoano.
