Na Hassan Kingu
Baada ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuipa tuzo klabu ya soka ya Simba, mashabiki wa soka nchini Tanzania waliingia katika mjadala mzito.
Mjadala wenyewe ni wa kuipinga BMT kwa kuipa Simba tuzo kwa kigezo gani, kabla ya kujua kigezo, mjadala ulipamba moto kwa mashabiki wa Simba na Yanga kuzodoana vijiweni na mitandaoni.
Mashabiki hasa wa Yanga waliamini timu yao ndiyo iliyokuwa na hadhi ya kupewa tuzo kutokana na mafanikio yake nchini Tanzania kuanzia mataji ya ligi kuu kwa misimu takriban minne na michuano mingine.
Kimsingi mjadala huu haukupaswa kuwapo lakini ulikuwapo kwa sababu ni hulka ya mashabiki wa timu hizi mbili hasimu kulumbana huku kila mmoja akiamini timu yake ndiyo bora kuliko mwenzake.
Nasema mjadala huu haukupaswa kuwapo kwa sababu tulikuwa tunabishana na kulumbana kwa jambo ambalo wengi wetu tulikuwa hatulijui na hatukusumbuka kulijua badala yake tuliendelea kusumbuka kwa kubishana na kulumbana.
Hatukuwa tunajua kigezo ambacho BMT ilitumia kuipa Simba tuzo hiyo, lakini tulichofanya ni kujiaminisha kuwa Yanga ni bora kuliko Simba na Simba ambao pia walikuwa hawajui kigezo cha BMT kuipa timu yao tuzo nao walijiaminisha kuwa timu yao ni bora kuliko Yanga.
Mjadala huu ulikufa baada ya BMT kuweka wazi kigezo kwamba wao waliangalia mafanikio ya timu kimataifa, Simba walikuwa hawajui kuhusu kigezo lakini waliitetea timu yao na Yanga walikuwa hawajui lolote kuhusu kigezo nao waliamini timu yao ni bora kuliko Simba.
Kumbe kilichotokea ni kwamba BMT waliwaza kimataifa wakati sisi akili zetu ziliwaza kishabiki tena jijini Dar es Salaam katika wilaya ya Ilala mitaa ya Msimbazi, Kariakoo na Twiga na Jangwani.
Tungejaribu kuwaza kimataifa kama BMT na kuwa na fikra na mitazamo ya kimataifa, mjadala huu au malumbano haya yasingekuwapo lakini hatukuwaza huko badala yake mawazo yetu yalikuwa Tanzania, si nje ya Tanzania.
Kwa maana nyingine BMT wao waliwaza mambo ya Cairo, Misri yalipo makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), waliwaza Rabat-Morocco, Lagos-Nigeria, Abidjan-Ivory Coast, Tunis-Tunisia na kwingineko lakini sisi fikra na mitazamo yetu iliishia kuwaza mitaa ya Jangwani na Twiga na Msimbazi na Kariakoo.
Na ndio maana sasa hivi hatusikii tena mjadala na malumbano kuhusu tuzo ya Simba, ni kwa sababu tulijadili na kulumbana tusichokijua, tumeujua ukweli tumeishia kubaki kimya na kuhamishia mijadala na malumbano yetu katika mambo mengine.
Kumalizika kwa malumbano na mjadala huo ni vyema kukawa somo kwa mashabiki wa soka nchini kuwa wadadisi wa mambo kabla ya kuanza kuyajadili tena kujadili kwa kutumia nguvu nyingi katika kushambuliana.
Ndio, kuitetea timu yako si jambo baya lakini lazima ujue unachotetea au kukipinga, je uko sahihi au unatetea na kupinga usichokijua, unatetea au kupinga tuzo ya Simba bila kujua kigezo ambacho kimetumika kutoa tuzo hiyo!
Makala Hapa BMT wametufikirisha kimataifa
Hapa BMT wametufikirisha kimataifa
Read also
