Foxborough, Mass
Kocha wa timu ya taifa ya Morocco, Mohamed Ouahbi amesema timu yao ipo pamoja na nahodha wao, Achraf Hakimi na kwamba mchezaji huyo yuko katika hali ya utulivu licha ya tuhuma za kubaka zinazomkabili.
Kauli ya kocha huyo imekuja baada ya mahakama moja ya rufaa ya Ufaransa kuthibitisha Ijumaa, Juni 18, 2026 kwamba mchezaji huyo anatakiwa mahakamani kwa kesi ya kubaka.
Siku ambayo uamuzi wa mahakama hiyo ulitangazwa, Hakimi alikuwa akijiandaa kuiongoza Morocco akiwa ndiye nahodha wa timu kwenye mechi ya fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Scotland, mechi ambayo Morocco walishinda kwa bao 1-0.
Februari mwaka huu, Hakimi ambaye pia ni beki wa PSG ya Ufaransa alipinga uamuzi wa jaji uliotokana na mapendekezo ya waendesha mashtaka waliotaka mchezaji huyo afikishwe mahakamani kwa kesi ya kubaka.
Alipoulizwa Ouahbi na waandishi wa habari iwapo anaguswa na kesi hiyo na kupata tabu kumsimamia Hakimi kwenye timu ya Morocco, kocha huyo alisema jambo hilo haliwasumbui na Hakimi yuko vizuri uwanjani.
“Uliangalia mechi, nafikiri uliangalia, Hakimi alikuwa wa kipekee uwanjani kwa hiyo tuko katika hali ya utulivu, ametulia na naamini alicheza vizuri sana,” alisema Ouahbi.
Baadhi ya mashabiki walikuwa wakimzomea Hakimi kila wakati alipougusa mpira ingawa hilo halikuonekana kumpa tabu mchezaji huyo ambaye amesisitiza kuwa hajafanya kosa lolote.
