Philadelphia, Marekani
Baada ya Brazil kuichapa Haiti mabao 3-0 katika mechi ya Kundi ya C ya fainali za Kombe la Dunia, kocha wa timu hiyo, Carlo Ancelotti amesema anatarajia nyota wake Neymar Jr atakuwapo dimbani Jumatano katika mechi dhidi ya Scotland.
Neymar, 34, amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya misuli ya nyuma ya paja na mara ya mwisho kuonekana uwanjani ilikuwa Mei 17, 2026 akiiwakilisha Santos katika mechi ya ligi nchini Brazil.
Kwa mujibu wa Ancelotti, Neymar anatarajia kufanya mazoezi pamoja na wachezaji wenzake Jumatatu, Juni 22, 2026 baada ya kuanza mazoezi ya peke yake hapo kabla.
Majeraha yalimfanya Neymar kukosa mechi za Brazil za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazoendelea lakini mchango wake ulikuwa mkubwa katika mechi alizocheza kwa kufunga mabao mawili na kutoa asisti tatu katika mechi nne.
Katika hatua nyingine, Ancelotti hakuweka wazi kama ataendelea kumpanga Matheus Cunha katika nafasi ya mshambuliaji wa kati licha ya kufunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza.
Cunha alianza badala ya Igor Thiago baada ya kuanzia benchi na kuingia uwanjani dakika ya 61 katika mechi ya kwanza ya Brazil dhidi ya Morocco ambayo iliisha kwa sare ya bao 1-1.
“Anaweza akacheza, nafikiri nafasi ya Matheus anakuwa vizuri katika kuwasumbua mabeki, na hata pasi zake anatoa vizuri na nafasi yake ni yenye kuleta usumbufu mbele, tutaangalia hilo,” alisema Ancelotti.
Brazil ndiyo inayoshika usukani kwenye kundi lake ikiwa na pointi nne sawa na Morocco ambao waliifunga Scotland bao 1-0 lakini Brazil ina faida ya mabao ya kufunga.
