Barcelona, Hispania
Barcelona au Barca Jumapili Mei 10, 2026 wametwaa taji la La Liga msimu wa 2025-26 baada ya kuwachapa mahasimu wao Real Madrid mabao 2-0, ushindi wenye maana kubwa kwa Marcus Rashford aliyefunga bao la kwanza.
Bao hilo la mpira wa adhabu limezidi kupaisha thamani ya Rashford ambaye ni kama amejifungulia njia katika kikosi cha timu ya taifa ya England kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026.
Rashford pia amejifungulia njia katika klabu, uwezekano wa kupewa mkataba wa kudumu Barca ni mkubwa au kurudi Man United, timu yake iliyomtoa kwa mkopo baada ya kupitia kipindi kigumu.
Mpira wa adhabu uliopigwa na mshambuliaji huyo umbali wa mita 20 ulionekana kumtatiza kipa wa Real Madrid, Thibaut Courtois ambaye aliishia kuungalia ukiingia wavuni juu kwenye kona ya kushoto.
Kasi ya mashambulizi ya Barca iliendelea na majibu yake yakapatikana kwa bao la pili mfungaji akiwa ni Ferran Torres ambaye alishirikiana vizuri na Dani Olmo hadi kufunga bao hilo.
Barca waliokuwa wenyeji wa mechi hiyo maarufu El Clasico inayozihusisha timu hizo mahasimu wa soka la Hispania, ushindi wao umewawezessha kubeba taji hilo mara ya pili mfululizo.
Kwa upande mwingine wamezidi kuwaacha pagumu mahasimu wao Real Madrid msimu huu tangu kuachana na kocha wao Xabi Alonso hadi kutolewa katika michuano mbalimbali ikiwamo Ligi ya Mabingwa Ulaya, michuano inayotajwa kuwa ya hadhi yao.
Zaidi ya hilo hali tete imeendelea kujitokeza miongoni mwa wachezaji wa timu hiyo kukiwa na abari kwamba wachezaji wamekuwa wakigombana wao kwa wao kila mmoja akijiona kuwa juu.
Matukio hayo yanaonekana kuongeza matatizo kwa kocha wa muda, Alvaro Arbeloa wakati mwenzake Hansi Flick akifurahia maisha katika kikosi cha Barca ambacho kimebeba taji kikiwa na mechi tatu mkononi.
Kinachoonekana Real Madrid ni kama vile timu imekuwa kubwa mno kwa Arbeloa, mastaa wamempanda kichwani na kuna kila dalili kwamba hatokuwa na timu hiyo msimu ujao.
Mmoja wa makocha ambaye jina lake limekuwa likitajwa kukabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo ni Jose Mourinho na kama hilo litafanikiwa basi kocha huyo maarufu Special One atakuwa anarudi katika timu hiyo kwa mara ya pili.
Kimataifa Barca yabeba taji La Liga
Barca yabeba taji La Liga
Read also
