Liverpool, England
Winga wa Liverpool, Mohamed Salah amesema kwa sasa yupo katika hali ya amani baada ya kukubali kuachana na klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu na kupata fursa ya kuangalia mambo yake mengine.
Salah atahitimisha safari yake ya miaka tisa ya mafanikio ikiwamo kuwa mfungaji bora wa klabu hiyo ya Anfield katika majira ya kiangazi msimu huu baada ya makubaliano ya kukatisha mkataba wake mnono wa miaka miwili aliosaini miezi 12 iliyopita.
Msimu huu haukuwa mzuri kwa mchezaji huyo na klabu kwa ujumla na zaidi ya yote ni tukio la Desemba mwaka jana pale alipotofautiana na kocha wake Arne Slot hasa alipomuweka benchi.
Hali ya amani baina ya wawili hao ilirejea baada ya Salah kurudi katika klabu hiyo akitokea kuiwakilisha timu yake ya taifa ya Misri kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Morocco.
“Nafikiri niendelee kwa msimu huu, hili ni jambo sahihi kulifanya kwa sasa na nina amani katika hilo, msimu ulikuwa mgumu kwetu sote, sitaki kusema mengi zaidi,” alisema Salah.
Salah alifafanua kuwa ana furaha kwa uamuzi huo wa kuondoka na kwa kila alichopitia msimu huu kinamfanya kukataa na kuamua kwamba ni muda wa kuondoka na kwa jambo hilo ana furaha.
Inadaiwa kwamba Salah pamoja na kuonekana anaondoka katika hali isiyo na amani lakini makubaliano ya pamoja yamepunguza tatizo na inatarajiwa ataagwa rasmi na kwa heshima anazostahiki.
