Tehran, Iran
Rais wa Shirikisho la Soka Iran (FFIRI), Mehdi Taj (pichani) amesema kwamba mwenyeji wao kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 ni Fifa si Marekani wala rais wa nchi hiyo, Donald Trump.
Iran imetaka heshima timu yake ikiwa nchini Marekani kwenye fainali za Kombe la Dunia ambazo zitaanza kutimua vumbi kuanzia Juni 11 mwaka huu katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.
Mehdi hivi karibuni alikuwa mmoja wa wajumbe wa Iran kwenye mkutano wa Fifa mjini Vancouver, Canada lakini walikwama kushiriki mkutano huo kwa kilichodaiwa kuwa ni kukosewa heshima na maofisa uhamiaji wa Canada.
Katika tukio hilo Mehdi na ujumbe wake waliamua kurudi Iran uamuzi ambao Mehdi ameutetea ingawa wizara ya mambo ya ndani ya Canada ilieleza kuwa visa ya kiongozi huyo wa Iran ilifutwa kwa sababu ya kuhusishwa kwake na kundi la Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC).
IRGC ni kundi maalum lililoanzishwa Iran kwa lengo la kulinda maslahi ya taifa hilo kisiasa, kiuchumi na katika nyanja mbalimbali na hadi sasa linafahamika kuwa kundi lenye nguvu za kijeshi.
Katika nchi za Marekani na Canada, IRGC ni kundi linalohusishwa na ugaidi na inadaiwa katika nchi hizo mtu yeyote mwenye ukaribu na IRGC haruhusiwi kuingia nchi hizo.
Mehdi kwa upande wake alisema wanachotaka ni kuhakikishiwa kwamba hawatakosewa heshima kwa namna yoyote ile ikiwamo kulidhalilisha kundi la IRGC ambalo alilitaja kuwa ni alama muhimu katika mfumo wa taifa la Iran.
Kiongozi huyo pia alisisitiza kuwa Iran imefuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia na inakwenda kushiriki na mwenyeji wao ni Fifa.
“Tunakwenda kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa sababu tumefuzu na mwenyeji wetu huko ni Fifa si Trump au Marekani,” alisema Mehdi.
Katika siku za karibuni kumekuwapo mjadala kuhusu hatma ya Iran na ushiriki wao kwenye fainali za Kombe la Dunia licha ya Rais wa Fifa, Gianni Infantino kusisitiza kuwa Iran itashiriki fainali hizo.
Iran imepangwa kucheza mechi zake mbili za awali mjini Los Angeles dhidi ya New Zealand na Ubelgiji, mechi ambazo zitachezwa Juni 15 na 21 na mechi yao ya mwisho ya makundi itakuwa Juni 26 dhidi ya Misri mjini Seattle.
Hali ya utata kuhusu hatma ya Iran kushiriki fainali hizo imejitokeza tangu kuibuka kwa vita ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
