Carlifonia, Marekani
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Argentina na klabu ya Inter Miami ya Marekani, Lionel Messi amesema Neymar Jr ni mmoja wa wachezaji bora duniani hivyo anatakiwa kuwa na timu ya Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Akifafanua hoja yake hiyo, Messi alisema wanataka wachezaji bora wawepo kwenye fainali hizo na Neymar bila kujali kiwango chake cha sasa wakati wote anabaki kuwa mmoja wa wachezaji bora.
Alisema litakuwa jambo la kipekee kumuona Neymar kwenye fainali za Kombe la Dunia akiwa na timu ya Brazil kwa sababu ya umuhimu wake kwa timu hiyo na soka kwa ujumla.
Messi hata hivyo alisema hawezi kuwa na uhakika wa moja kwa moja kwa sababu tu wakati wote mchezaji huyo anatakiwa kuwa katika mashindano kama hayo.
“Neymar ni rafiki yangu, hilo lipo wazi na ningependa awepo kwenye Kombe la Dunia kwa sababu mambo mengi yatajitokeza kwake kwa kuwa ana haki hiyo kwa namna alivyo na natumaini atakuwapo,” alisema Messi.
Messi, 38 na Neymar 34, wamekuwa marafiki tangu wacheze pamoja katika klabu ya Barcelona ya Hispania kwa misimu minne na baadaye kuwa pamoja PSG ya Ufaransa kwa misimu miwili.
Wachezaji hao waliondoka pamoja PSG mwaka 2023, Messi ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Argentina alihamia Inter Miami na Neymar alijiunga na klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia.
Neymar hata hivyo baada ya kucheza Al Hilal na kupata majeraha, alirudi Brazil akajiunga na klabu ya Santos takriban mwaka mmoja uliopita akipambana kurudi katika ubora akiwa na matarajio ya kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya nne.
