Munich, Ujerumani
Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, PSG wamefuzu kwa mara ya pili mfululizo hatua ya fainali ya ligi hiyo baada ya kuibwaga Bayern Munich na sasa wanasubiri kuumana na Arsenal.
PSG wakiwa ugenini Allianz Arena katika mechi ya nusu fainali iliyopigwa Jumatano Mei, 6, 2026 walilazimisha sare ya bao 1-1 kwa wenyeji Bayern.
Kwa matokeo hayo, PSG wamekata tiketi ya kucheza fainali kwa ushindi wa jumla ya mabao 6-5 baada ya kupata ushindi wa mabao 5-4 katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo.
PSG, wababe kutoka Ufaransa sasa wanasubiri kuikabili Arsenal katika fainali itakayopigwa Mei 30, 2026 mjini Budapest, mechi itakayoamua kama PSG watatwaa taji mara ya pili mfululizo au Arsenal watafanya yao.
Kufuzu fainali kwa mara ya pili mfululizo ni tukio kubwa si kwa mashabiki, wachezaji na benchi la ufundi la PSG linaloongozwa na kocha Luis Enrique, bali hata rais wa klabu hiyo, Nasser Al-Khelaifi hakusita kuonesha furaha yake kwa mafanikio hayo.

“Ni jambo la kipekee, fainali mara ya pili, na sasa tutakwenda pale na kujaribu kuisaka nyota ya pili, niliwaambia wachezaji sisi ni mashujaa,” alisema Al-Khelaifi.
Wakati, PSG wakisaka taji mara ya pili mfululizo, Arsenal chini ya kocha Mikel Arteta wao wamezika unyonge wa muda mrefu kwa kufikia hatua ya fainali, mara ya mwisho kufikia hatua hiyo ilikuwa mwaka 2006.
Kilichobaki kwa Arteta ni kufungua ukurasa mpya kwa kulibeba taji hilo, ubora wa timu hiyo msimu huu unatoa kila ishara kwamba inawezekana kubeba taji hilo msimu huu ingawa jibu sahihi litapatikana Mei 30, 2026.
