Na mwandishi wetu
Wachezaji Clatous Chota Chama wa Simba na Allan Okelo wa Yanga wameibuka mashujaa katika Ligi Kuu NBC kwa kila mmoja kufunga bao pekee na kuipa timu yake ushindi wa bao 1-0.
Katika mechi hizo zilizochezwa Jumatano Mei 6, 2026, Yanga wakiwa kwenye dimba la KMC Mwenge, Dar es Salaam dhidi ya KMC walipata bao lao pekee dakika ya 65 lililofungwa na Okelo.
Okelo, nyota kutoka Uganda, alifunga bao hilo pekee kwa shuti kali la nje ya eneo la penalti baada ya kuinasa pasi ya Shekhan Ibrahim.
Yanga kwa kiasi kikubwa waliutawala mchezo na kufanikiwa kulinda bao hilo na kupata matokeo ambayo yamewawezesha kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kukusanya pointi 51 katika mechi 21.
Nao Simba waliokuwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo dhidi ya JKT Tanzania walipata bao lao pekee na la ushindi katika dakika ya 55.
Chama, nyota kutoka Zambia ambaye pia alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi hiyo ikiwa ni mara ya pili mfululizo, kama kawaida yake alionesha utulivu kabla ya kupiga shuti ambalo lilikwenda moja kwa moja hadi wavuni.
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 46 ikiendelea kukomaa katika nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 21 kama mahasimu wao Yanga.
Kimataifa Chama, Okelo wazibeba Simba Yanga
Chama, Okelo wazibeba Simba Yanga
Read also
