Na mwandishi wetu
Uongozi wa Yanga umetangaza kumtimua kocha wake mkuu, Pedro Concalves na kwa kipindi hiki hadi mwisho wa msimu timu itakuwa chini ya makocha Abdihamid Moalim na Patrick Mabedi.
Taarifa ya mtendaji mkuu wa klabu hiyo iliyopatikana leo Jumatano Mei 6, 2026 imemshukuru Pedro kwa kipindi chote ambacho amekuwa na timu hiyo na kumtakia kila la heri katika majukumu yake yajayo.
Yanga katika taarifa hiyo hata hivyo haikuweka bayana nini hasa sababu ya kufikia uamuzi wa kuachana na Pedro lakini inadhaniwa kuwa mwenendo wa timu hiyo haukuwa ukiwafurahisha viongozi.
Kabla ya mechi yao ya fainali ya Kombe la Muungano dhidi ya mahasimu wao Simba iliyochezwa Aprili 29, 2026, kulikuwa na fununu za kocha huyo kutimuliwa.
Pedro hata hivyo alikuwa na timu hiyo lakini mwisho wa siku walishindwa kutamba baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 na uvumi wa kutimuliwa ukaibuka tena kwa kasi.
Simba walicheza mechi nyingine na Yanga Mei 3, 2026, mechi ya Ligi Kuu NBC na kutoka sare ya mabao 2-2 na mara baada ya mechi hiyo habari za kutimuliwa kocha huyo ziliibuka tena kwa kasi zaidi.
Katika habari hizo ilikuwapo moja ya uwongo kwenye mitandao ya jamii ikiuhusisha uongozi wa Yanga na uamuzi wa kumtimua kocha huyo lakini hakukuwa na ukweli wowote hadi ilipotoka taarifa rasmi ya leo.
Pedro kocha ambaye anatokea nchini Ureno, alianza rasmi kuinoa Yanga Oktoba mwaka jana akiichukua timu kutoka kwa Roman Folz.
Kimataifa Kocha Pedro atimuliwa Yanga
Kocha Pedro atimuliwa Yanga
Read also
