Na mwandishi wetu
Kocha msaidizi wa Singida Fountan Gate, Nizar Khalfan (pichani) amesema matokeo mabaya wanayoyapata kwenye mechi za hivi karibuni yamechangiwa na kuondoka kwa baadhi ya wachezaji muhimu wa kikosi cha kwanza.
Nizar alisema hayo leo Jumapili na kufafanua kuwa wachezaji waliopo si kwamba hawana uwezo bali wanakosa muunganiko wa kucheza pamoja kitu ambacho kinawasumbua na kusababisha wakose matokeo mazuri.
Baadhi ya wachezaji walioondoka kwenye dirisha dogo ni washambuliaji tegemeo Elvis Rupia na Marouf Tchakei, pia yupo Duke Abuya wote wamejiunga na Ihefu FC.
Wengine ni Gadiel Michael ametimkia Cape Town Spurs ya Ligi Kuu Afrika Kusini pamoja na Meddie Kagere ambaye amejiunga na Namungo FC.
“Tumewapoteza wachezaji muhimu kwenye dirisha dogo, kwa kiasi fulani kumeiyumbisha timu ndio maana hatupati ushindi, wachezaji waliopo wanapambana lakini wanakosa muunganiko,” alisema Nizar.
Kocha huyo alisema kama benchi la ufundi hali hiyo inawaumiza lakini wanaendelea kupambana kuhakikisha timu hiyo inapata muunganiko wake haraka na kufanya vizuri mechi zinazokuja.
Alisema pamoja na kutopata matokeo lakini kwa kiasi fulani wanaridhishwa na upambanaji wa wachezaji wao katika mechi zote walizocheza tangu kuanza kwa mzunguko wa pili na wanachokitafuta hivi sasa ni ushindi wa kwanza ili kuwajengea hali ya kujiamini.
Singida ambayo kwa sasa inautumia Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kama uwanja wake wa nyumbani imeendelea kuporomoka kutoka nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC.
Kwa sasa timu hiyo ipo nafasi ya nane kwenye ligi hiyo kutoka ya tano ilipokuwepo mwishoni mwa mzunguko wa kwanza.
