Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka la ufukweni, Boniface Pawasa amesema baada ya miaka miwili ya kushiriki michuano ya Baraza la Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa) na kukosa ubingwa, awamu hii wamejipanga kurudi na kombe.
Katika miaka miwili waliyoalikwa, mwaka wa kwanza walifika fainali na kutolewa na Msumbiji na mwaka jana walitolewa hatua ya nusu fainali na Senegal hivyo hii ni mara ya tatu watashiriki mashindano hayo yanayotarajia kuanza Machi 17 hadi 25, mwaka huu.
Akizungumzia maandalizi ya timu hiyo jijini Dar es Salaam Alhamisi hii, Pawasa alisema baada ya kufanya mazoezi ya kwenda na kurudi kwa zaidi ya wiki moja, Ijumaa hii wataingia kambini rasmi kufanya maandalizi ya mwisho.
“Lengo letu msimu huu ni kwenda Afrika Kusini na kurudi na kombe, tunaendelea vizuri na maandalizi, wachezaji wako vizuri kwa mapambano,” alisema beki huyo wa kati wa zamani wa Simba SC na Taifa Stars.
“Kwa kipindi chote tulichoshiriki tumekuwa wanafunzi bora, kama benchi la ufundi tumeimarika, nayahimiza makampuni mbalimbali kujitokeza kuiunga mkono timu na sisi tunawaahidi mwaka huu tunakwenda kupeperusha vyema bendera ya Tanzania,” alisema Pawasa.
