Munich, Ujeumani
Kocha anayejiandaa kuondoka katika klabu ya Bayern Munich, Thomas Tuchel amesema kwamba yeye si mtu pekee wa kulaumiwa kwa kiwango kibovu cha timu hiyo msimu huu wa 2023-24.
Akizungumza Ijumaa hii Tuchel pia alisema kwamba uamuzi wa klabu hiyo kuachana naye mwishoni mwa msimu huu unampa uhuru katika maamuzi atakayofanya kwa kipindi chote kilichobaki.
Bayern hivi karibuni ilitangaza kuvunja mkataba na Tuchel mwishoni mwa msimu ingawa mkataba wa kocha huyo unafikia ukomo Juni 2025, chanzo cha kumvunjia mkataba kinaaminika kuwa ni matokeo mabovu vikiwamo vipigo vitatu mfululizo katika mechi za mashindano tofauti.
“Sidhani kama mimi ndio tatizo pekee lakini nakubali kubeba lawama, sijaridhika namna tunavyocheza na kwa kipindi kirefu sikuwa mwenye kufurahishwa, sasa tuko katika hatua nyingine tofauti, utata umeondolewa na tumefikia makubaliano lakini bado sidhani kama tatizo ni mimi peke yangu,” alisema Tuchel.
Katika Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’, Bayern yenye rekodi ya kubeba taji la ligi hiyo kwa misimu 11 mfululizo, mambo yake si mazuri msimu huu ikiwa imeachwa na vinara wa ligi hiyo, Bayer Leverkusen kwa tofauti ya pointi nane.
“Haijalishi kama nimeuelewa uamuzi wa klabu au ninaufurahia, jambo pekee la msingi kwa sasa ni kwamba kuna kitu kipo wazi, uwazi unakupa uhuru na hilo ni jambo zuri katika mechi na mazoezi,” alisema Tuchel.
Tuchel ambaye timu yake Jumamosi hii itaumana na RB Leipzig katika mechi ya Bundesliga, aliongeza kwamba kilichotokea ni kumpa kocha uhuru zaidi wa kufanya kazi.
Alisema kwamba kwa sasa hawezi tena kuanza kufikiria matokeo ya mbeleni kwa uamuzi atakaoufanya na kwa kiasi fulani anaweza kuwa na ujeuri katika kufanya maamuzi anayoamini.
